VIJANA wawili wanaojihusisha na ufundi ujenzi kwenye maeneo mbalimbali, ikiwamo viwandani wametekwa na watu wasiojulikana usiku wa kuamkia Feb 4, mwaka huu, huko Miembesaba Mjini Kibaha, Pwani.
Vijana hao ambao ni Abdul Ratwifu Kassimu na Abdul Rahman, walitekwa wakiwa katika nyumba waliyopanga huko mtaa wa Miembesaba B, Kata ya Kongowe, Wilaya ya Kibaha.
Mmoja wa mashuhuda amesema tukio hilo limetokea usiku wa saa saba watu wote wakiwa wamelala na alianza kusikia mbwa wakibweka, huku watu wakitembea nje ya nyumba hiyo.
Amesema alipochungulia dirishani aliona watu sita mmoja akiwa na bunduki wakielekea moja kwa moja kwenye chumba wanapoishi vijana hao na kugonga, ili wafunguliwe.
Amesema watu watatu kati ya sita waliingia ndani, baada ya kufunguliwa na vijana hao, huku watatu wakibaki nje kuimarisha ulinzi.
Amesema muda mfupi baadae walitoka ndani wakiwa na vijana hao, huku wamewafunga pingu na kutokomea kusikojulikana.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED