Aua shemeji yake, mwingine mke atoa taarifa

By Ida Mushi , Nipashe
Published at 04:50 PM Feb 20 2025
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, SACP Alex Mkama
PIcha: Mtandao
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, SACP Alex Mkama

MKAZI wa Kijiji cha Malulu wilayani Kilosa, mkoani Morogoro, Festo Makambula (35), anashikiliwa na Polisi Mkoa Morogoro, akituhumiwa kumuua mlinzi wa kampuni ya Stigmaltin, na kumchoma kisu kifuani na kusababisha kifo chake baada ya kumvamia na kumshambulia.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, SACP Alex Mkama, amesema mauaji hayo yametokea Februari 18, 2025 majira ya asubuhi huko katika eneo la Mululu, Kisanga ambapo mtuhumiwa alimshambulia Rashid Bandei Kiupi(49) ambaye ni shemeji yake wakati akielekea kazini na kumuua.

Akasema uchunguzi wa awali umebaini kuwa chanzo cha tukio hilo ni ugomvi unaohusiana na mahusiano ya mapenzi kati ya marehemu na dada wa mtuhumiwa na kwamba hatua za upelelezi zinakamilishwa, ili mtuhumiwa afikishwe kwenye vyombo vya vingine katika mnyororo wa haki jinai.

Katika tukio lingine, Philibert Mtamiela (52), mkulima na mkazi wa kijiji cha Tangihuru wilayani Malinyi, mkoani Morogoro, amekutwa amekufa kwa kujinyonga kwa kutumia kamba ya viatu akiwa ndani ya kibanda kinachotumiwa kwa shughuli za shamba.

Kamanda Mkama alisema mwili huo umekutwa porini na inadaiwa kabla ya kifo chake alikuwa akitafutwa kwa tuhuma za kumuua mke wake kwa kutumia silaha nyenye makali, kwa kumpiga sehemu ya kichwani.

Kamanda huyo wa Polisi akasema mwamaume huyo baada ya kuhakikisha amemuua mkewe, alipiga simu kwa ndugu mbalimbali akiwafahamisha kuwa amemuua mkewe kwa sababu kuchoshwa na matatizo mbalimbali aliyokuwa akiyafanya mkewe.