Baadhi ya wanawake waliopata huduma ya kujifungua katika Kituo cha Afya Mkoani, Kibaha, wamepongeza huduma bora zinazotolewa huku wakiomba wahudumu wengine kwenye wodi ya wazazi kuwa wanyenyekevu zaidi ili kuondoa malalamiko kwa serikali.
Wanawake hao wamesema kuwa unyenyekevu wa madaktari na wauguzi katika kituo hicho umevutia wengi kutoka maeneo mbalimbali, hata nje ya Mkoa wa Pwani.
Amina Rashid, mkazi wa Kiluvya, Dar es Salaam, amesema aliamua kujifungulia katika kituo hicho licha ya kuwepo vituo vya afya karibu naye kutokana na huduma bora anazosikia kutoka kwa waliowahi kutibiwa hapo.
"Nilikuja hapa kwa sababu madaktari na wauguzi wanawahudumia wagonjwa kwa heshima na kuwashauri vizuri," amesema Amina.
Naye Honorina Denis, mkazi wa Kibamba, amesema alichagua kituo hicho baada ya kupata ushuhuda mzuri kutoka kwa ndugu yake, hali iliyomfanya kuacha vituo vingine na kuhamia huko kwa huduma ya kujifungua.
Mganga Mfawidhi wa kituo hicho, Dk. Abdulkadir Sultani, amesema kituo hicho kilichoanzishwa kama zahanati mwaka 1983, kilipandishwa hadhi kuwa kituo cha afya mwaka 2015.
Tangu mwaka huo, idadi ya wanawake wanaojifungua imeongezeka kwa kasi.
“Tunajitahidi kutoa huduma bora na tunawaahidi wanawake wote kuwa tutazidi kuboresha huduma zetu,” amesema.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED