Amuua rafiki yake kwa kumtwanga ngumi kichwani

By Nebart Msokwa , Nipashe
Published at 05:19 PM Feb 20 2025
Ngumi.

Musa Basuka (30) mkazi wa Kitongoji cha Manyanya katika Mamlaka ya Mji Mdogo wa Makongolosi Wilaya ya Chunya mkoani Mbeya, anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kumuua rafiki yake kwa kumtwanga ngumi kichwani.

Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, Kamishna Msaidizi wa Polisi Wilert Siwa ameyasema hayo alipozungumza na wandishi wa habari kuhusu oparesheni zinazofanywa na jeshi hilo katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo.

Amesema mtuhumiwa alimuua rafiki yake aitwaye Issa Mohamed (30) ambaye alikuwa mchimbaji mwenzie wa madini ya dhabu baada ya kutokea mabishano yaliyosababishwa na zamu ya kupika.

“Hawa watu walikuwa wanakaa chumba kimoja na tukio hili la mauaji lilitokea Februari 18 jioni baada ya kutokea mabishano ya zamu ya kupika ambapo marehemu alitakiwa kupika na mtuhumiwa alitakiwa kuchota maji,” amesema Siwa

Kamanda Siwa amewataka jeshi hilo linaendelea na uchunguzi wa tukio hilo na kwamba ukikamilika mtuhumiwa atafikishwa mahakamani kwa hatua za kisheria huku akiwataka wananchi kuacha kujichukulia sheria mkononi.