Kijiji cha Mkupuka, kilichopo wilayani Kibiti, mkoani Pwani, ni miongoni mwa vijiji 57 vinavyonufaika na mpango wa matumizi ya ardhi, hatua inayolenga kudhibiti migogoro ya ardhi na kuboresha matumizi ya rasilimali hiyo.
Mpango huo unatekelezwa na Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi kwa kushirikiana na Halmashauri za Wilaya sita nchini. Lengo kuu ni kutatua changamoto mbalimbali za ardhi zinazovikumba vijiji husika.
Akizungumza wakati wa utekelezaji wa mpango huo, Ofisa Mipango Miji na Vijiji ambaye pia ni Mratibu Mkuu wa mpango huo katika ngazi ya Halmashauri, Ovodius Kahangwa, amesema hatua hiyo itasaidia kumaliza migogoro ya ardhi katika vijiji lengwa na kuweka msingi wa maendeleo endelevu.
Naye, Mkuu wa Kanda ya Mashariki wa Tume hiyo na msimamizi wa mpango huo katika Mkoa wa Pwani, Edward Mpanda, ameeleza kuwa uandaaji wa mpango wa matumizi ya ardhi unafanyika kwa njia shirikishi kuanzia ngazi ya mkoa hadi vijiji. Aliongeza kuwa, kwa Kijiji cha Mkupuka, ambacho kinajulikana kwa uzalishaji mkubwa wa mazao ya kibiashara kama korosho, mpango huo utasaidia kuongeza thamani ya ardhi na kuimarisha maendeleo ya kiuchumi.
Baadhi ya wakazi wa kijiji hicho, akiwemo Magdalena Lukas, wameipongeza Serikali kwa mpango huu, wakisema utakuwa msaada mkubwa katika kumaliza migogoro ya ardhi ya muda mrefu na kutambua maeneo yenye thamani kwa ajili ya maendeleo ya jamii.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED