Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Saad Mtambule amezitaka taasisi zinazofanya kazi ndani ya wilaya hiyo kuiga mfano wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) ya kuwashirikia viongozi wa Serikali za mitaa kwenye utekelwzaji wa majukumu yao.
Amesema hatua hiyo itawasadia viongozi hao kuwa na uelewa mpana wa kile kinachofanyika ili nao wakawasilishe kwa wananchi juu ya yale yanayofanywa na Serikali yao.
Mtambule amesema hayo Jumatatu ya Februari 17, 2025 katika ziara iliyoandaliwa DAWASA yenye lengo la kushirikisha viongozi hao juu ya utekelezaji wa shughuli za utoaji wa huduma ya Majisafi kwa wananchi wa Dar es Salaam.
"DAWASA ni Taasisi ya mfano katika Wilaya ya Kinondoni na Dar es Salaam kwa ujumla, katika Wilaya ya Kinondoni ni sehemu chache sana zenye changamoto ya upatikanaji wa Majisafi, maeneo mengi huduma ya Majisafi inafika na kwa uhakika, napenda kuwapongeza sana Taasisi hii kwa jitihada hizi," ameeleza.
Mwakilishi wa Afisa Mtendaji , Mkurugenzi wa Uzalishaji na Usambazaji maji kutoka DAWASA, Mhandisi Leonard Msenyele amesema ziara hiyo ni mahususi kwa lengo la kuwawezesha viongozi wetu ambao wako karibu na Wananchi waweze kujua hatua mbalimbali zinazohusika katika uzalishaji na usambazaji wa maji kutoka Mtamboni.
"Viongozi hawa tumewaita kutoka katika Mitaa ya Manispaa ya Kinondoni, ili waweze kufikisha ujumbe kwa wananchi," ameeleza Mhandisi Msenyele.
"Tumeandaa ziara hii kwa Wenyevitii kwa kutambua umuhimu wao katika maeneo tunayoyahudumia, kwani wao ndio wamekuwa karibu sana na Wananchi na endapo kutakuwa na changamoto yoyote basi wasikie uchungu na kile ambacho tunakipoteza," ameongeza Mhandisi Msenyele.
Amesema DAWASA imejipanga vyema katika kutoa huduma kwa jamii ikiwa ni pamoja na kuongeza mtandao wa maji kwa maeneo ambayo yana changamoto ya huduma ya maji.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Kisiwani, Athumani Issa ameipongeza DAWASA kwa ziara hii na kutambua nafasi zao katoka huduma itolewayo kwa kuwa wamejifunza kwani wametoa dhana mbaya iliyokuwapo vichwani mwao.
“Ziara hii imenifunza mengi sana na kuanzia sasa sitaruhusu kuona jamii ikiwa inapoteza maji kwa kuwa Serikali inatumia gharama kubwa kuhakikisha wananchi wanapata huduma,” ameeleza Mwenyekiti Issa
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED