DCEA yakamata dawa za kulevya, silaha na pembe ya ndovu Arusha

By Zanura Mollel , Nipashe
Published at 02:31 PM Feb 18 2025
DCEA yakamata dawa za kulevya, silaha na pembe ya ndovu Arusha.
Picha: Mpigapicha Wetu
DCEA yakamata dawa za kulevya, silaha na pembe ya ndovu Arusha.

Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Aretas Lyimo, amesema kuwa katika operesheni maalum iliyofanyika mkoani Arusha, mamlaka hiyo ilifanikiwa kukamata pembe moja ya ndovu pamoja na risasi 11 za moto.

Aidha, katika tukio jingine mkoani humo, mtu mmoja alikamatwa akiwa ameotesha miche ya bangi ndani ya nyumba yake kwa kutumia glasi za plastiki (disposable). Kamishna Lyimo amebainisha kuwa biashara haramu ya dawa za kulevya mara nyingi inahusiana na uhalifu mwingine, ikiwa ni pamoja na usafirishaji haramu wa silaha.

Katika kipindi cha Januari hadi Februari 2025, DCEA ilikamata jumla ya kilogramu 98.55 za bangi, kilogramu 162.111 za mirungi, gramu 301 za heroin na gramu 195 za dawa zingine za kulevya mkoani Arusha.

Mamlaka hiyo imeendelea kuhimiza ushirikiano kutoka kwa wananchi katika vita dhidi ya biashara haramu ya dawa za kulevya na uhalifu unaoambatana nayo.