IBADA NYUMBANI: Askofu, familia watoa angalizo kwa Lissu

By Elizabeth Zaya , Nipashe
Published at 08:54 AM Feb 18 2025
MAKAMU Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Singida, Padre Francis Lyimu (kulia) na Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo Taifa (CHADEMA), Tundu Lissu.
Picha: Nipashe Digital
MAKAMU Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Singida, Padre Francis Lyimu (kulia) na Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo Taifa (CHADEMA), Tundu Lissu.

MAKAMU Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Singida, Padre Francis Lyimu, amesema Mungu ana kusudi na Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo Taifa (CHADEMA), Tundu Lissu na kumtaka aendelee kumtegemea Mungu.

Padre Lyimu alitoa kauli hiyo jana wakati wa misa maalum ya shukrani na ya kumwombea mwanasiasa huyo nguli nchini iliyofanyika kijijini kwa wazazi wake, Mahambe wilayani Ikungi mkoani Singida na kuhudhuriwa na wakazi wa kijiji hicho na wanachama wa CHADEMA waliosafiri kutoka mikoa mbalimbali nchini.

"Ukimtegemea Mungu utapita kwenye shida ya maradhi au kukosa mahitaji mengine, lakini hawezi kukuacha. Na ndiyo maana huyu ndugu yetu (Lissu) amekuja kushukuru leo maana Mungu hakumwacha, risasi hizo zote mpaka sasa bado yuko na sisi.

"Mungu hawaachi wanaomcha. Mheshimiwa (Lissu), endelea kumtegemea Mungu, ana kusudi na wewe na kama ilivyo, kila mmoja ameletwa duniani kwa makusudi yake, kila mmoja amebeba ujumbe wa Mungu," Padre Lyimu alisema.

Kiongozi huyo wa dini alisisitiza neno lake kwa kuwataka watu kumtegemea na kumcha Mungu na kutenda haki, huku akikemea tabia ya ubinafsi kwa kauli kwamba "ni jambo baya na linamchukiza Mungu".

Padre Lyimu alisema: "Upendo ambao Mungu ametupatia, tushukuru. Mahali pengine wakati huu ni vita, ni mitutu, unasikia mirindimo ya risasi, lakini sisi tunakaa, tunamcha na kumwabudu Mungu katika hali ya amani na utulivu.

"Kwani tumechoka na utulivu, tumechoka na amani? Ninaomba tuendelee kumcha Mungu, tuendelee kuwaombea hawa wenzetu ambao wana nia njema ya kutaka kujitoa sadaka kwa ajili ya wengine, kila mmoja tuombe neema ya kujitoa sadaka kwa ajili ya wengine bila ya kujihurumia.

"Tumwombe Mungu kwa ajili ya taifa letu, atusaidie sisi sote tutende haki, tuwe watu wa shukrani na tumwombe atusaidie tusije tukaingia kwenye ole, tunapopata ridhiki, tunapofanikiwa, tugawane na wengine lakini ubinafsi wa kujilimbikizia mali na kuwadhulumu wengine ni kosa kubwa mbele ya Mungu," Padre Lyimu alionya.

Akitoa neno la shukrani kwa niaba ya familia, Alute Mughwai, kaka wa Lissu, alisema familia yao iko tayari kumuunga mkono ndugu yao huyo katika harakati zake za kupigania haki kwenye mambo mbalimbali, zikiwamo rasilimali asili za nchi pamoja na demokrasia, lakini wako tayari pia kumkosoa pale watakapoona anakengeuka.

"Baadhi ya viongozi wetu wanakosolewa kwa habari ya kuhubiri amani zaidi kuliko kuhubiri haki. Haki ikiwapo, amani itafuata na bila shaka sisi wana ukoo na wanakijiji kwa ujumla, wenye mapenzi mema, tumekuunga mkono ndugu yetu (Lissu) na tutaendelea kukuunga mkono kwenye juhudi zako hizi.

"Na tutakuwa wa kwanza kukukosoa na 'kukurudi' pale ambapo utaacha kupigania misingi hii, au pale ambapo utakapokubali kutekwa na ‘machawa’ ukalewa na madaraka. Ukifanya hivyo, tutakurudi na tutakuwa wa kwanza kufanya hivyo," Mughwai alionya.

Kaka huyo wa Lissu alizungumzia pia baadhi ya kauli na mashambulizi ambayo yamekuwa yanaelekezwa kwa mdogo wake huyo kupitia mitandao ya kijamii.

"Wapinzani wake watasema 'amefanya nini Mahambe mnamfanyia sherehe mtu huyu ambaye ni mkorofi?' Sisi tutatabasamu... wabaya wake wamesema na wataendelea kusema kwamba, 'Bwana Lissu ni mtu asiye na heshima kwa wengine, ni mgomvi na kwa hivyo asisikilizwe katika harakati zake za kupigania uhuru, ulinzi wa rasilimali asilia na demokrasia ya kweli katika nchi hii'.

"Sisi tunaomfahamu tutatabasamu na kuwauliza 'je, kuna yeyote kati yenu aliyemshuhudia ndugu yetu akimshambulia mtu yeyote shambulio la kudhuru mwili? Kuna mtu ambaye alimwona huyu bwana amekwangua mtu yeyote katika maisha yake?' Sisi tunamfahamu zaidi," alisema.

Mughwai alisema wao, familia, wanaendelea kumwombea ndugu yao huyo ili Mungu ampe baraka kuijenga kesho bora ya Tanzania.

"Je, kuna kosa lolote la jinai ambalo huyu bwana alishtakiwa, kutiwa hatiani na kufungwa? Je, mlijaribu kumsikiliza kwa makini mambo anayopigania? Kama mlimwona na kumsikiliza kwa umakini, mngemfahamu na mngejua ni kwa nini sisi wana-Mahambe tumeamua kwa dhati kabisa kumpa heshima hii, na kwa nini tunamwomba Mungu ampe baraka zote na nguvu ya kushiriki katika kuijenga kesho bora ya nchi hii.

"Ninasema hivyo kwa sababu jukumu la ujenzi wa jamii inayofuata misingi ya uhuru, demokrasia, haki, udugu na amani ni la kila mmoja wetu," Mughwai alisema.

Lissu alichaguliwa Januari 21, mwaka huu kushika nafasi ya Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, akimshinda mtangulizi wake Mbowe katika uchaguzi ulioibua mvutano mkubwa ndani ya chama hicho kikuu cha upinzani nchini.

OOOO