BWAWA LA NYERERE: Serikali yaanza mchakato wa kushusha bei ya umeme

By Ashton Balaigwa , Nipashe
Published at 08:02 AM Feb 18 2025
Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, aki-zungumza na waandishi wa habari katika Mradi wa Bwawa la kufua Umeme la Julius Nyerere (JNHPP), Rufiji, mkoani Pwani jana, kuhusu maendeleo ya mradi ambao tayari ujenzi wake umefikia asilimia 99.8.

SERIKALI imesema ujenzi wa Mradi wa Bwawa la Kufua Umeme la Julius Nyerere (JNHPP) umekamilika kwa asilimia 98.8 na unazalisha zaidi ya Megawatt 1,880.

Kutokana na utekelezaji wa mradi huo, imesema inaangalia uwezekano wa kupunguza gharama za umeme baada ya kukamilisha kuchakata na kuona uwiano wa fedha zilizotumika kwenye ujenzi huo.

Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, alisema hayo jana wakati akijibu maswali ya waandishi wa habari kwenye mkutano wa kueleza utekelezaji wa kazi mbalimbali kwenye eneo la Bwawa la Mwalimu Nyerere lililoko mikoa ya Pwani na Morogoro.

"Kwa sababu nimesema Bwawa la Nyerere limekamilika, kwa hiyo kiu kubwa ya watanzania wengi wangependa bei ya umeme ishuke kesho, watanzania subirini kidogo, tumetumia fedha hapa, wataalam wetu watachakata, tutaendelea kuangalia uwiano kwa kuwa bado tunazalisha kwenye vyanzo vingine.

"Lakini mkumbuke fedha hizi tumezichomoa na kusimamisha mambo mengine, ni lazima twende 'tunajibalansi' lakini tutafika hatua ambazo tutapunguza gharama za umeme, itakapofika tutawajulisha," alisema.

Msigwa ambaye ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, alisema Tanzania ni moja ya nchi zenye gharama za chini za umeme barani Afrika zinazochangia kupatikana kwa wawekezaji kutoka sekta binafsi kwa kuwa wanapenda kuwekeza katika sehemu ambazo watapata faida.

"Wakija kuwekeza Tanzania kwa sababu serikali imewekeza katika umeme na gharama wanazotozwa wananchi ni za chini, wamekuwa wakidai wanapata changamoto ya biashara hailipi. 

"Kwa hiyo watanzania msiwe wanyonge, umeme wetu ni wa gharama nafuu sana lakini tunatambua baada ya uwekezaji huu tuliofanya, tutafika mahali gharama za umeme zitapungua tu," alisema Msigwa.

Akizungumzia mradi huo wenye thamani ya Sh. trilioni 6.558 na uwezo wa kuzalisha Megawati 2,115 ulioanza mwaka 2019, Msigwa alisema kuwa hadi Februali 15, 2024, ujenzi ulikuwa umefikia asilimia 98.8 na mashine nane kati ya tisa zimeshawashwa na kufanya jumla ya megawati 1,880 kuongezeka kwenye Gridi ya Taifa.

"Hapa upo mtambo wa tisa wa kuzalisha umeme ambapo kila mtambo una uwezo wa kuzalisha Megawati 235 na kwa ujumla wake zinazalisha Megawati 2,115 na tayari imekamilika na kituo cha kupokea na kusafirisha umeme wa JNHPP na kuingiza kwenye Gridi ya Taifa kimekamilika kwa asilimia 100," alisema Msigwa.

Alisema mtambo namba moja uliobaki kati ya tisa uko katika hatua za mwisho za usimikaji na unatarajia kuanza majaribio mwishoni mwa mwezi Februari wakati mradi wa kusafirisha umeme kutoka JNHPP hadi Chalinze – kV 400, njia yenye urefu wa kilomita 160, umefikia asilimia 99.5 kulinganishwa na asilimia 44 mwaka 2020/21.

Msigwa alisema hadi sasa mkandarasi ameshalipwa zaidi ya Sh. trilioni 6.5 sawa na asilimia 95.90 na kiasi kidogo kilichobaki kimewekwa kwa ajili ya dharura baada ya kukamilika kama sehemu ya matazamio ya mradi huo.

SOKO LA UMEME

Akizungumzia mafanikio ya Mkutano wa Nishati wa Wakuu wa Nchi za Bara la Afrika ambao Tanzania ilikuwa mwenyeji, Msigwa alisema ulikuwa na ajenda ya kuwapatia umeme Waafrika milioni 300 ifikapo mwaka 2030 na umevutiwa na wadau wa maendeleo duniani.

Alisema wadau wa maendeleo wametoa ahadi za fedha nyingi ambazo zitawasaidia Waafrika zaidi ya 550 kuunganishwa umeme kati ya Waafrika wote milioni 600 na kwamba Tanzania inajiandaa kuwa soko la umeme kuziuzia nchi jirani.

Aliwataja wadau hao ni pamoja na Benki ya Dunia (WB) kupitia mpango wa nishati Afrika (Energy Compact) ambao benki hiyo imeahidi kutoa Dola za Marekani bilioni 22, Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) Dola za Marekani bilioni 18.2, Benki ya Maendeleo ya Kiislam Dola za Marekani bilioni 2.7 na Benki ya Maendeleo ya Asia Dola za Kimarekani bilioni 1.5.

Wengine ni Benki ya Maendeleo ya Ufaransa Dola za Marekani bilioni moja, Mfuko wa Maendeleo wa OPEC Dola za Marekani bilioni moja na Serikali ya Ufaransa Dola za Marekani bilioni moja.

Alisema kuwa Februari 21 na 22 mwaka huu, Tanzania itakuwa mwenyeji wa Mkutano wa Tatu wa Afrika wa Kahawa G25, utakaofanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam.

Alisema mkutano huo wa siku mbili utazikutanisha nchi 25 za Afrika zinazozalisha kahawa na utaanza na mkutano wa mawaziri Februari 21, 2025 na kufuatiwa na mkutano wa wakuu wa nchi Februari 22, 2025.

Alisema nchi za Afrika ambazo ni wazalishaji kahawa zinakutana kwa lengo la kujadiliana na kukubaliana kuhusu mwelekeo wa zao hilo katika Bara la Afrika kwa kuzingatia kuwa kahawa ni bidhaa ya nne katika biashara kubwa duniani baada ya mafuta, dhahabu na gesi asilia.

"Biashara ya kahawa duniani ina thamani ya Dola za Marekani bilioni 500 ambapo kati ya hizo mchango wa soko la Afrika ni Dola za Marekani bilioni 2.5. Kwa upande wa Tanzania katika soko hilo imepata Dola za Marekani milioni 240 kutoka milioni 170 za miaka mitatu iliyopita," alisema.

Msigwa alisema takwimu za sasa zinaonesha kuwa kuna nchi 50 zinazozalisha kahawa duniani ambapo kati ya hizo, bara la Afrika lina nchi 25.

Kwa upande wa Tanzania, uzalishaji kahawa ndani ya kipindi cha miaka mitatu umeongezeka kutoka tani 55,000 hadi tani 85,000.

Alisema Tanzania imechaguliwa kuwa mwenyeji wa mkutano huu katika Bara la Afrika kutokana na kupiga hatua kubwa katika uzalishaji zao hilo. Katika kipindi cha miaka mitatu, bei ya kahawa kwa wakulima imeimarika huku uzalishaji wake ukiongezeka pia. Mkutano huo utawakutanisha wasimamizi wa sera, wafanyabiashara na kampuni kubwa za kahawa.