Waasi wa M23 wauteka Mji wa Bukavu, wazidi kusonga mbele Kivu Kusini

By Maulid Mmbaga , Nipashe
Published at 04:53 PM Feb 18 2025
Waasi wa M23 wauteka Mji wa  Bukavu, wazidi kusonga mbele Kivu Kusini.
Picha: Mtandao
Waasi wa M23 wauteka Mji wa Bukavu, wazidi kusonga mbele Kivu Kusini.

Waasi wa M23 wanaendelea kupanua himaya yao katika Jimbo la Kivu Kusini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), baada ya kuuteka mji wa Bukavu na kusonga mbele kuelekea njia kuu zinazounganisha jimbo hilo na maeneo mengine ya nchi.

Taarifa zinaeleza kuwa waasi hao wanajipanga kudhibiti barabara ya taifa namba tano, inayounganisha Bukavu na wilaya za Uvira na Fizi hadi Jimbo la Tanganyika.

Jana, mapigano makali yaliripotiwa katika kijiji cha Nyangezi, kilicho kwenye barabara hiyo, kati ya waasi wa M23—wanaodaiwa kuungwa mkono na Rwanda—dhidi ya Jeshi la Kongo (FARDC), likisaidiwa na jeshi la Burundi pamoja na wapiganaji wa kundi la Wazalendo.

Mashuhuda wanasema kuwa baada ya saa kadhaa za mapigano, majeshi ya FARDC na askari wa Burundi walijiondoa kimkakati kutoka eneo hilo, hali iliyosababisha taharuki kwa wakazi wa Nyangezi. Wengi walilazimika kujifungia ndani ya nyumba zao, huku wengine wakikimbilia vijiji jirani kutafuta hifadhi.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa wakazi wa eneo hilo, baada ya kutwaa Nyangezi, waasi wa M23 waliendelea kuelekea vijiji vilivyopo kusini mwa bonde la Mto Ruzizi.

Jérémie, mkazi wa Kamanyola—eneo lililo mpakani mwa Kongo, Rwanda, na Burundi—amesema hali ya taharuki imeongezeka, huku wakazi wakihofia mapigano zaidi na uwezekano wa mji wao pia kutekwa.

Hali inazidi kuwa tete katika Kivu Kusini, huku jumuiya ya kimataifa ikiendelea kufuatilia kwa karibu mwenendo wa mgogoro huo.