Simba yaifuata Al Ahly Tripoli kibabe

By Faustine Feliciane ,, Shufaa Lyimo , Nipashe
Published at 10:29 AM Sep 11 2024
Meneja Habari na Mawasiliano wa klabu hiyo, Ahmed Ally.
Picha: Mtandao
Meneja Habari na Mawasiliano wa klabu hiyo, Ahmed Ally.

KIKOSI cha wachezaji 18 wa Simba kimeondoka nchini alfajiri ya leo kuelekea Libya tayari kwa mchezo wa kwanza wa raundi ya kwanza wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Al Ahly Tripoli.

Akizungumza na Nipashe jana, Meneja Habari na Mawasiliano wa klabu hiyo, Ahmed Ally, alisema wachezaji 18 wataondokea hapa nchini na wengine wanne ambao wapo kwenye majukumu ya Timu za Taifa za Tanzania na Guinea, wataungana na wenzao Libya moja kwa moja kesho wakitokea kwenye timu zao.

"Kikosi kipo tayari, kinaondoka kesho (leo) alfajiri, Libya tutakuwa na wachezaji 22, wengine wanne watakuja kuungana na sisi moja kwa moja Libya baada ya kumaliza majukumu yao kwenye timu zao za taifa," alisema Ahmed.

Aidha, alisema kocha wa timu hiyo, Fadlu Davids, amesema kikosi kimekamilika na wamejiandaa vizuri kupata ushindi kwenye mchezo huo wa ugenini.

"Kwenye mazoezi ya mwisho kocha ameridhishwa na maandalizi, wachezaji wake wapo kwenye morali kubwa kuelekea kwenye mchezo huo, kwa kifupi Wanasimba tuna matumaini makubwa na kikosi chetu kuelekea kwenye mchezo huo.

"Wachezaji wetu wapo vizuri kuelekea kwenye mchezo huo ambao tunaamini utakuwa na upinzani mkubwa, lakini kwa upande wetu tupo vizuri idara zote," aliongeza Ahmed huku akibainisha kuwa malengo yao ni kwenda kufanya vizuri na kuweza kuipeperusha vema bendera ya Tanzania kupitia mchezo wao huo. 

Alisema Fadlu amekuwa wakiwapa wachezaji mazoezi ya nguvu ambayo anaamini yameimarisha miili ya wachezaji kuelekea mchezo huo. 

Alisema morali ya kila mchezaji ipo juu katika kuhakikisha wanafanya vizuri na kusonga mbele kwenye mashindano hayo ili kutimiza malengo yao. 

Wachezaji wa Simba ambao wataenda kuungana na kikosi hicho wakitokea moja kwa moja kwenye majukumu ya timu zao za taifa ni Mohamed Hussein 'Tshabalala', Ally Salim na Edwin Balua ambao wapo na kikosi cha Taifa Stars.

Mwingine ni kipa Moussa Camara ambaye yupo na kikosi cha Guinea ambacho jana kilikuwa kikicheza na Taifa Stars mchezo wa kufuzu fainali za Afrika Mataifa ya Afrika (AFCON) zitakazofanyika nchini Morocco hapo mwakani.

Mchezo huo wa Kundi H, ambao Guinea ni mwenyeji, ulichezwa jana saa 1:00 usiku nchini Ivory Coast kutokana na viwanja vya wenyeji kutokidhi vigezo vya Shirikisho la Soka Afrika, CAF.

Mchezo wa kwanza wa Taifa Stars uliochezwa Uwanja wa Benjamin Mkapa wiki iliyopita dhidi ya Ethiopia, Stars ililazimishwa suluhu baada ya kumaliza dakika 90 bila kufungana dhidi ya Ethiopia.