Simba SC yaizima Mashujaa Kigoma

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 01:47 PM Nov 02 2024
Straika wa kimataifa kutoka Uganda, Steven Mukwala.
Picha: Mtandao
Straika wa kimataifa kutoka Uganda, Steven Mukwala.

STRAIKA wa kimataifa kutoka Uganda, Steven Mukwala, aliwapa furaha wanachama na mashabiki wa Simba, alipofunga bao pekee dakika za majeruhi dhidi ya Mashujaa FC katika mchezo mgumu wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliochezwa kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika mkoani, Kigoma jana.

Ikiwa baadhi ya mashabiki wa Simba waliokuwa uwanjani na waliokuwa wanafuatilia mechi hiyo kupitia redio walijua mchezo huo ungeisha kwa suluhu, lakini mambo yalibadilika sekunde chache kabla ya kipenga cha mwisho.

Baada ya mwamuzi, Omari Mdoe, kuongeza dakika sita, zilicheza na ilipotimu dakika ya mwisho Simba ilipata kona mbili mfululizo ambazo zote zilipigwa na Awesu Awesu aliyeingia kipindi cha pili, moja ikiokolewa na ya pili ikizaa bao lililowapa Wekundu wa Msimbazi pointi tatu muhimu.

Mukwala aliingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Fabrice Ngoma, aliruka juu zaidi ya wachezaji wote na kuunganisha kwa  kichwa mpira wa kona na kutinga wavuni na kuwaacha wachezaji wa Mashujaa, benchi la ufundi na mashabiki wao wasiamini kilichotokea.

Ni bao la pili kwa straika huyo kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu, moja akilifunga Agosti 25, mwaka huu kwenye Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam, Simba ilipocheza dhidi ya Fountain Gate na kupata ushindi wa mabao 4-0.

Ushindi wa jana umeipekeleka Simba hadi nafasi ya pili ikifikisha pointi 22 baada ya kucheza michezo tisa, ikishinda saba, sare moja na kupoteza mmoja, ikipachika mabao 17 na kuruhusu matatu.

Imeishusha Singida Black Stars yenye pointi 22 hadi nafasi ya tatu, ikiathiriwa na kufunga mabao 13 ambayo ni machache kuliko Simba.

Dakika ya pili tu ya mchezo, Leonel Ateba alianza kulisabahi lango la Mashujaa, lakini shuti lake la mguu wa kushoto lilipaa juu.

Mashujaa ilijibu shambulizi hilo dakika sita baadaye pale, Yusuph Dunia alipoambaa kwenye wingi ya kulia na kupiga krosi iliyoleta kizaazaa katika lango la Simba kabla ya Shomari Kapombe kuamua kuutoa mpira nje na kuwa kona.

Faulo ya moja kwa moja ya Kibu Denis nje ya eneo la hatari dakika ya 11, ilipanguliwa na kipa wa Mashujaa, Erick Johora na kuwa kona ambayo pia ilileta hatari tena, Kibu kwa mara ya pili alikaribia kufunga kwa kichwa, lakini mpira huo aliounganisha kwa kichwa ukapaa juu ya lango.

Dakika tisa baadaye Simba ilirejea tena kwenye lango la Mashujaa ambapo kama wachezaji wake, Ngoma, Kibu na Ladack Chasambi wangetulia wangeweza kuipatia timu yao mabao.

Ilikuwa ni krosi ya mguu wa kushoto ya Ateba, ambayo ilizua patashika nguo kuchanika langoni mwa Mashujaa, lakini wachezaji hao hawakuitendea haki.

Joshua Mutale ambaye alikuwa katika kiwango cha juu jana, aliwapiga chenga mabeki wa Mashujaa dakika ya 34 kabla ya kuachia shuti ambalo lilitoka pembeni mwa lango.

Kipindi chote cha kwanza, Simba ilitawala mpira kwa kiasi kikubwa, lakini Mashujaa walionekana kuweka viungo wakabaji wengi katikati ambao walivuruga mipango ya Simba, pia hawakuwaacha wapinzani wao wawe na utulivu pale wanapopata mpira.

Kipindi cha pili Mashujaa FC waliamua kukaa nyuma kulinda lango lao na walitumia muda mrefu kuokoa, kupiga mipira mirefu wakishambulia kwa kushtukiza mara chache na kupoteza muda.

Kipigo hicho kimeibakisha Mashujaa na pointi zake 13 ikiwa nafasi ya saba ya msimamo wa Ligi Kuu, ikiwa imecheza mechi tisa.