Serikali kukusanya bilioni 200/- michezo kubashiri

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 09:46 AM Jul 22 2024
Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Michezo ya kubashiri nichini (GBT), James Mbalwe.
Picha: Mtandao
Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Michezo ya kubashiri nichini (GBT), James Mbalwe.

JUMLA ya Sh. bilioni 200 zinatarajiwa kukusanywa kupitia michezo ya kubashiri ifikapo mwishoni mwa mwaka wa fedha wa 2024, imeelezwa.

Hayo yalisemwa na Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Michezo ya kubashiri nichini (GBT), James Mbalwe, wakati wa uzinduzi wa Kampuni mpya ya Michezo ya Kubashiri ya Betwinner jijini Dar es Salaam jana.

Mbalwe alisema kiwango hicho cha fedha ni ongezeko la Sh. bilioni 30 kulinganishwa na makusanyo ya mwaka jana ambayo yalikusanya jumla ya Sh. bilioni 170.

Alisema kuwa sekta ya Michezo ya Kubashi (Sports Betting), kwa sasa inakuwa kiasi cha kuchangia katika mfuko wa taifa na kukuza uchumi wa nchi.

“Sekta ya 'Sports Betting', imepata maendeleo makubwa na kuwa na mchango mkubwa katika kuchangia mfuko wa taifa. Hivyo ujio wa Kampuni ya Betwinner, itaungana na kampuni nyingine kuchangia mfuko wa taifa.

Natoa wito kwa makampuni kuwa waadilifu, kuwa na weledi na uwazi katika kufanya shughuli zake ili kujipatia wateja na kuendelea kukua,” alisema Mbalwe.

Alisema ujio wa kampuni hiyo utaleta chachu ya maendeleo ya michezo hiyo hapa nchini mbali ya kuleta ushindani.

Kwa upande wa Mwenyekiti wa Shirikisho la Kampuni za Michezo ya kubashiri Tanzania (TSBA), Sabrina Msuya, aliipongeza kampuni hiyo kwa kuingia katika soko la Tanzania.

"Nawapongeza kwa kuingia katika soko la Tanzania na kuendeleza sekta hii ambayo kwa sasa inakua kwa kasi,” alisema Msuya.

Naye Mkurugenzi wa Masoko wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Aaron Nyanda, alitoa wito kwa kampuni hiyo kusaidia ligi zao mbalimbali ikiwa pamoja na Championship na nyinginezo.

Pia aliipa angalizo kampuni hiyo kutotumia katika matangazo picha za wachezaji ambao hawana haki nazo ili kuepuka kuingia katika kesi ambazo zimetokea tayari na kampuni nyingine kushindwa.

Kwa upande wa Mkurugenzi Mkuu wa Betwinner, Jesse Ndambala, alisema wanafuraha kubwa kuingia nchini na kuchangia pato la taifa huku wakiwa na malengo mengine mbalimbali ikiwa ni pamoja na kusaidia maendeleo ya michezo na jamii.

Ndambala alisema ujio wao umelenga kuwapa wateja 'odds' nzuri zaidi tofauti na kampuni nyingine za kubashiri.

Alisisitiza kuwa wameleta ubunifu mkubwa katika michezo yao ya kubashiri ikiwa ni pamoja na kuwapa asilimia 100 ya bonasi kwa wateja wapya ikiwa ni sehemu ya ofa ya ukaribisho.

"Mbali na kuwa na odds nzuri, tumeweka ubunifu mkubwa katika michezo yetu na kutoa asilimia 100 ya bonasi kwa wateja wapya. Lengo hapa ni kuongeza burudani na chachu ya ushindani kwenye sekta ya michezo.

"Mbali na soka, pia tutaangalia jinsi gani ya kuwekeza katika michezo mbalimbali kama gofu, netiboli na mingineyo," alisema Ndambala.