Ruvu Shooting yashuka tena daraja

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 05:22 PM Apr 26 2024
Timu ya Ruvu Shooting.
Picha: Maktaba
Timu ya Ruvu Shooting.

TIMU ya Ruvu Shooting imeshuka daraja baada ya kutoka suluhu dhidi ya Transit Camp katika mechi ya Ligi ya Championship katika mechi iliyochezwa Uwanja wa Samora, Iringa.

Timu hiyo sasa itashiriki Ligi Daraja la Pili 'first league', msimu ujao baada ya kuteremka kutoka Ligi ya Champioship, msimu mmoja tu baada ya kushuka kutoka Ligi Kuu Tanzania Bara.

Ruvu Shooting ilishuka daraja kutoka Ligi Kuu, msimu wa uliopita wa 2022/23 na msimu wa kwanza tu kucheza Championship, imeshindwa kuhimili vishindo na sasa imeshuka tena.

Timu hiyo imeshuka kwa kuwa ina pointi 13 mpaka sasa na inashika mkia, ikibakisha mechi moja tu dhidi ya Green Warriors, ambayo hata kama ikishinda itakuwa na pointi 16 ambazo tayari zimeshapitwa na Pam African, yenye pointi 19.

Pan, ambayo ilishinda mabao 2-1 dhidi ya Biashara United wiki hii, ilifikisha idadi hiyo ya pointi na  kuhitimisha safari ya Ruvu Shooting.

Hata hivyo, Pan African, Mabingwa wa Tanzania Bara mwaka 1982, haiko salama kwani wanahitaji ushindi katika mechi yao ya mwisho Jumapili ijayo dhidi ya Stand United, Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Mbweni, Dar es Salaam.

Timu hiyo yenuye pointi 19, ikishinda itafikisha pointi 22, ambazo zinamilikiwa na Copco inayoshika nafasi ya 14.

Iwapo Copco itatoka sare katika mechi yake ya mwisho dhidi ya TMA kesho, katika mechi inayotarajiwa kuchezwa, Uwanja wa Black Rhino, Karatu, Arusha, Pan African nayo itaungana na Ruvu Shooting kushuka daraja kwenda 'first league'.