Pamba yaweka vikao kujadili vipigo Ligi Kuu

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 11:40 AM Oct 11 2024
Ofisa Habari wa klabu hiyo yenye maskani yake jijini Mwanza, Moses William.
Picha: Mtandao
Ofisa Habari wa klabu hiyo yenye maskani yake jijini Mwanza, Moses William.

BAADA ya kufanya vibaya kwenye michezo yake saba ya mwanzo ya Ligi Kuu Tanzania Bara, viongozi na benchi la ufundi la Pamba Jiji FC wamekuwa katika vikao kujadili mwenendo huo na kuangalia nini cha kufanya ili kujikwamua.

Ofisa Habari wa klabu hiyo yenye maskani yake jijini Mwanza, Moses William, alithibitisha kuwapo kwa vikao hivyo ambavyo amevitaja vimekuwa vyenye tija na manufaa kwa maslahi mapana ya timu hiyo.

Pamba Jiji ambayo imepanda daraja msimu huu, ndiyo timu pekee ambayo haijashinda mchezo wowote wa Ligi Kuu Tanzania Bara mpaka sasa kati ya mechi saba ilizocheza, ikiburuza mkia na pointi zake nne.

"Kimsingi kulikuwa na vikao vya hapa na pale kufanya tathmini ya mwenendo ya klabu baina ya benchi la ufundi na manejimenti.

Vikao hivyo vimekuwa na tija na vimekuwa na manufaa kimsingi na maslahi mapana na Pamba Jiji.

Haya matokeo tuliyoyapata yanatukumbusha kuwa sisi tupo wapi na tunatakiwa tufanye nini, imekuwa vizuri kwamba ni mapema kwa hiyo tunayo nafasi ya kusahihisha makosa, tuwaambie mashabiki wetu kwamba ni kweli tumeanza vibaya ila hatuna timu mbaya, ni ubora wa wapinzani wetu, kwani tumekutana na ratiba ngumu mwanzoni mwa ligi," alisema ofisa habari huyo.

Katika michezo yake saba iliyocheza, imetoka sare michezo minne na kupoteza mitatu, huku mchezo uliopita ilipokea kipigo cha mabao 4-0 kutoka kwa Yanga, mchezo uliochezwa, Oktoba 3, mwaka huu kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.

Mbali na hilo, amesema tayari wachezaji wa timu hiyo wamesharejea mapumzikoni na kuanza mazoezi kujiandaa na mchezo utakaofuata dhidi ya Kagera Sugar, utakaochezwa Oktoba 21, mwaka huu kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.

"Nadhani baada ya vikao mambo yataenda kama tulivyotarajia, lakini pia baada ya ratiba ngumu ya kucheza na timu ya Singida Black Stars, Yanga, Prisons, Mashujaa, tutaanza kufanya vizuri," alisema.