SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema inatarajia kujenga uwanja mwingine mkubwa wa kisasa wenye hadhi ya kimataifa utakaotumika kwenye fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027, ambapo Tanzania, Kenya na Uganda zitakuwa mwenyeji wa fainali hizo kwa mara ya kwanza.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, ndiye aliyetoa kauli hiyo wakati akiweka jiwe la msingi kwenye ujenzi wa viwanja vipya vya michezo, Maisara (Maisara Sports Complex), Wilaya ya Mjini, Mkoa wa Mjini Magharibi, ikiwa ni mwendelezo wa shamrashamra za miaka 61 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Rais Dk. Mwinyi alisema serikali imelenga kujenga viwanja vya kisasa vya michezo kila wilaya pamoja na akademi za michezo (Sprots Academy) kila mkoa.
“Tuna dhamira ya kweli ya kujenga uwanja wa kisasa wa AFCON utakaofanana na ule wa Old Trafford wa Manchester United ya Uingereza,” alisisitiza Rais Dk. Mwinyi.
Alisema serikali pia inakusudia kufanya marekebisho makubwa ya viwanja vya Gombani Kisiwani Pemba na Uwanja wa Mao Tse Tung, Unguja lengo likiwa ni kuwa na viwanja vya kisasda vyenye hadhi vitakavyokuwa chachu ya kuwainua vijana kimichezo.
Aliongeza kuwa dhamira nyengine ya serikali ni kujenga uwanja wa soka la ufukweni (Beach soccer) kwa hadhi ya kimataifa na kujenga bwawa kubwa la kuogelea (Swimming Pool) lenye hadhi ya Olympic, (Olympic size Swimming Pool).
Alibainisha kuwa kwa muda mrefu amekuwa akisononeshwa kwa kuwapo viwanja vibovu vyenye vumbi na matope ambavyo vijana walivitumia kuchezea michezo mbalimbali ikiwamo soka, hali ambayo imepitwa na wakati, hivyo serikali imejiandaa kujenga viwanja vipya ili kutoa fursa kwa vijana kuinua vipaji vyao na ushindani kimataifa.
Alisema bado Zanzibar ina nia ya kurudi tena kuwa mwanachama wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF), hivyo ujenzi wa viwanja hivyo ni itakuwa chachu na kutoa ushawishi wa kupata uanachama huo.
Dk. Mwinyi alisema kuna kila sababu kwa Zanzibar kuwa mwanachama wa CAF kwa sababu ina timu mahiri ya “Zanzibar Heroes” inayoweza kuleta ushindani na vikombe nchini.
Alisema, lengo ni kuongeza vipaji ili Zanzibar iwe mshindani kimataifa katika nyanja mbalimbali za michezo.
Akizungumzia kuhusu Uwanja mpya wa Maisara (Maisra Sports Complex) aliowekea jiwe la msingi, Dk. Mwinyi aliishukuru Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, kwa kusimamia ipasavyo maendeleo ya ujenzi huo ambao kwa kiasi kikubwa utaimarisha sekta ya hiyo nchini.
Pia, Dk. Mwinyi alisema kuwapo kwa viwanja vya mpira wa kikapu (basket ball), mpira wa wavu (volleyball), mpira wa mikono (hand ball) na mchezo wa 'Long tennis' kutatoa mazingira bora kwa vijana kujifundisha michezo hiyo na kuzalisha vipaji zaidi.
Aidha, alifurahishwa na kuwapo kwa kituo cha mazoezi ya viungo uwanjani hapo (fitness center) pamoja na viwanja vya kufurahishia watoto (Children playground).
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED