NBC yafurahia 'Derby' ya Kariakoo, yajivunia Ligi Kuu

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 10:29 AM Oct 21 2024
Mkurugenzi wa Fedha wa Benki ya NBC Rayson Foya (kulia) akikabidhi tuzo ya Mchezaji Bora (Man of the match) kwa mchezaji Maxi Nzengeli kutoka klabu ya Yanga SC aliyeibuka mchezaji bora wa mchezo kati ya Simba SC na Yanga SC maarufu kama ‘Kariakoo Derby.
Picha:Mpigapicha Wetu
Mkurugenzi wa Fedha wa Benki ya NBC Rayson Foya (kulia) akikabidhi tuzo ya Mchezaji Bora (Man of the match) kwa mchezaji Maxi Nzengeli kutoka klabu ya Yanga SC aliyeibuka mchezaji bora wa mchezo kati ya Simba SC na Yanga SC maarufu kama ‘Kariakoo Derby.

WAKATI mechi ya ‘Kariakoo Derby’ Simba na Yanga, ikipigwa katika Uwanja wa Benjamin Mkapa juzi na kusisimua mashabiki wengi kutokana na soka la uhakika lililotandazwa, Mdhamini Mkuu wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Benki ya Taifa ya Biashara (NBC), ilifanikiwa kuipamba na kuandaa matukio kadhaa kwa ajili ya wapenzi wa mchezo huo pamoja na wateja wao.

Matukio hayo yalilenga kutoa fursa kwa wadau hao kukutana pamoja, ili kuutazama na kufurahia vizuri zaidi mchezo huo ambao ulimalizika kwa Yanga kushinda bao 1-0 katika dakika ya 86 lililopatikana kwa beki wa Simba Kelvin Kijili kujifunga wakati akiwa kwenye harakati za kuokoa.

Pamoja na kuandaa chakula cha mchana kwenye hotel ya Four Points iliyopo jijini Dar es Salaam, mahususi kwa baadhi ya wateja wake wanaoshabikia timu hizo mbili, mdhamini huyo pia aliwawezesha kwenda Uwanja wa Benjamin Mkapa wakiwa kwenye msafara maalum, ili kushuhudia mechi hiyo wakiwa kwenye jukwaa la VIP. 

Shughuli zote hizo ziliongozwa na maofisa waandamizi wa benki hiyo wakiongozwa na Mkurugenzi wa Fedha, Rayson Foya, ambaye pia alipata wasaa wa kukabidhi tuzo kwa Mchezaji Bora wa Mchezo (Man of the Match), Maxi Nzengeli, kutoka Klabu ya Yanga, tukio lililoshuhudiwa na maelfu ya mashabiki waliofika uwanjani hapo na wengine wengi waliokuwa wakitazama mchezo huo kupitia matangazo ya moja kwa moja ya televisheni.

Zaidi, benki hiyo iliandaa ‘screen’ kubwa kwenye baadhi ya maeneo ya Jiji la Dar es Salaam, ikiwamo katika mgahawa maarufu wa Hoppipola uliopo Masaki, ili kutoa fursa kwa mashabiki wengi zaidi ambao hawakupata wasaa wa kufika uwanjani waweze kushuhudia vizuri mechi hiyo kubwa zaidi nchini Tanzania na Ukanda wa Afrika Mashariki kwa ujumla.

Awali, akizungumzia hatua hiyo wakati wa hafla ya chakula cha mchana na wateja wao, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Mahusiano ya Umma wa NBC, Godwin Semunyu, alisema ni mwendelezo wa maadhimisho ya mwezi wa huduma kwa wateja wa benki hiyo, sambamba na jitihada zao kama mdhamini mkuu wa ligi hiyo kuutumia mchezo pendwa wa soka kujenga mahusiano na wateja wao sambamba na kuchochea mapenzi ya wadau hao kwa klabu zao na mchezo huo kwa ujumla.

“Udhamini wetu kwenye mchezo huu pendwa zaidi nchini na duniani kwa ujumla, umekuwa hauishii tu kulenga katika kuboresha ligi hizi tatu tunazozidhamini, bali pia tumekuwa tukihakikisha wadau wetu wote muhimu wakiwamo wafanyakazi, uongozi wa benki na wateja wetu wanakuwa sehemu ya mchezo huu kwa kushiriki moja kwa moja kwenye matukio mbalimbali, ikiwamo kushuhudia mechi kubwa kama hizi,” alisema Semunyu.

Zaidi, benki ya NBC iliandaa ‘screen’ kubwa kwenye baadhi ya maeneo ya jiji la Dar es Salaam ikiwemo kwenye Mgahawa maarufu wa Hoppipola uliopo Masaki ili kutoa fursa kwa mashabiki wengi zaidi ambao hawakupata wasaa wa kufika uwanjani waweze kushuhudia vizuri mechi hiyo kubwa zaidi nchini Tanzania na ukanda wa Afrika Mashariki kwa ujumla.

Alisema benki hiyo inaendelea kubuni mikakati mikubwa zaidi ya kuiboresha ligi hiyo, ili kufikia malengo ya udhamini wake ambayo ni pamoja na kukuza vipaji na viwango vya soka nchini, kuchochea ajira kupitia michezo, kuongeza ushindani baina klabu zinazoshiriki na kuongeza hamasa ya mchezo huo nchini.

“Kila mtu ni shuhuda wa mapinduzi makubwa ambayo tayari benki ya NBC tumeyafanya katika misimu hii mitatu iliyopita ya udhamini wetu kwenye Ligi Kuu ya NBC na mwaka mmoja wa udhamini wetu kwenye Ligi ya Championship na Ligi ya Vijana,” alisema.

Mbali na kuchochea ushindani kwenye ligi hizo kupitia udhamini ulioziwezesha klabu shiriki kufanya usajili mzuri, imeshuhudiwa mdhamini huyo pia akitoa huduma muhimu za kibenki kwa timu hizo, ikiwamo bima za afya, mikopo ya usafiri kwa timu na kushiriki katika kudhamini hafla mbalimbali za mchezo huo, zikiwamo zile za kukabidhi vikombe vya ubingwa pamoja na kudhamini tuzo mbalimbali za mchezo huo.