Mkude: Simba, Yanga zinafanana

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 11:24 AM Oct 11 2024
Mkude: Simba, Yanga zinafanana
Picha:Mtandao
Mkude: Simba, Yanga zinafanana

WAKATI Kocha Mkuu wa Simba, Fadlu Davids, amebadili aina ya mazoezi katika kikosi chake kuelekea mechi ya watani wa jadi, kiungo mkabaji wa Yanga, Jonas Mkude, amesema mazingira na maisha katika klabu mbili kongwe nchini, yanafanana.

Simba na Yanga zinatarajia kukutana katika mchezo wa mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu Tanzania Bara Oktoba 19, mwaka huu kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Wakizungumza jijini wachezaji wa Simba, Edwin Balua, Mzamiru Yassin na Yusuph Kagoma, wamesema wamekuwa katika  maandalizi 'makali' ya kujiandaa na mchezo huo kwa sababu wamechoshwa na 'uteja'.

Balua aliliambia gazeti hili kocha wao Fadlu, pamoja na benchi la ufundi,  wamewabadilishia aina ya mazoezi kwa sababu wanahitaji kuona wameimarika huku akikiri mechi hiyo haitakuwa nyepesi.

"Hautakuwa mchezo mwepesi kwa sababu ni dabi, tumejiandaa vizuri, kama sisi wachezaji tumeanza maandalizi makali kuelekea kwenye mchezo huo. Kuna maandalizi ya tofauti kabisa, programu zimebadilika na hii inahusiana na mchezo huo, ila kwetu sisi hakuna kitu ambacho ni kigeni kwenye aina ya mazoezi hayo," alisema winga huyo aliyesajiliwa dirisha dogo msimu uliopita akitokea Tanzania Prisons.

Mzamiru kwa upande wake alisema hakuna dabi ambayo ni rahisi, lakini kwa upande wao wamejiandaa si kushinda mechi hiyo tu, bali kutwaa ubingwa msimu huu kwa sababu wamechoshwa na uteja wa misimu mitatu mfululizo.

"Kwa msimu huu tumejiandaa na vitu vingi, kuwafunga Yanga na ubingwa, ni msimu wa tatu hatupati chochote, sisi kama wachezaji tumechoshwa na uteja, ndiyo maana unaona msimu huu maandalizi yamekuwa makubwa mno," alisema Mzamiru.

Naye Kagoma, aliyesajiliwa msimu huu akitokea Fountain Gate, amesema ameshangazwa na mazingira aliyoyakuta kwenye klabu yake mpya ambapo ni tofauti na alipotoka.

Kagome ameeleza kufurahishwa na mazingira ya kambi, pamoja na ushirikiano mzuri anaopata kutoka kwa wachezaji wenzake.

"Mimi mchezaji aliyenishangaza sana nilipomwona kwa mara ya kwanza mazoezini kutokana na uwezo wake ni Joshua Mutale, na kambini kwetu kama asipokuwepo kila mtu anajua hayupo kwa sababu ni mwongeaji sana, humu kambini mchezaji ambaye ni mchekeshaji sana ni Kelvin Kijili na Ali Salim yeye huwa anawahi sana kwenye chakula," Kagoma alisema.

Akizungumza na gazeti hili jana, Mkude ambaye alijiunga na Yanga msimu uliopita akitokea Simba, alisema alichogundua  timu hizi mbili zinafanana na mambo mengi ikiwa ni pamoja na aina ya maisha na mazingira ya kambi huku mashabiki wao wanazifanya ziwe klabu zenye ushawishi mkubwa.

"Mimi siyo mchezaji wa kwanza kutoka Simba kuja Yanga, vile vile kuna wachezaji ambao wametoka Yanga kwenda Simba, ukikaa nao watakwambia hivi hivi, ni majina tu ndiyo yanabadilisha, hizi ni timu kubwa ambazo aina yao ya kambi, usafiri, benchi la ufundi na uongozi vinafanana na kwa bahati nzuri mimi sijacheza timu nyingine zaidi ya hizi mbili," alisema Mkude ambaye ni zao la kikosi cha pili cha Simba.

Kiungo huyo ambaye alikuwa na uhakika wa namba katika kikosi cha kwanza cha Wekundu wa Msimbazi alisema timu hizo mbili zinabebwa na mtaji mkubwa wa  mashabiki, bila wao ni kama hakuna kitu.

"Mashabiki ndiyo watu wanaweza kufanya mpira kuwa rahisi kwenye timu, ukiangalia mashabiki wa Yanga wamekuwa ni watu wenye sapoti kubwa sana na timu yao, na hata mashabiki wa Simba kwa upande wao ni watu ambao wanapenda timu yao, yaani hizi timu mbili bila mashabiki hakuna kitu," alisema Mkude.

Kuhusu mchezo wa dabi utakaochezwa Oktoba 19, mwaka huu, Mkude alisema hajawahi kuwa na presha katika mchezo wowote unaozikutanisha timu hizo.

Aliongeza kama akipata nafasi basi mashabiki wataona kitu ambacho atafanya, kwa sababu yeye ndiyo atakuwa mmoja wa wachezaji watakaocheza dabi nyingi zaidi pamoja na Mohamed Hussein 'Zimbwe Jr' pamoja na Shomari Kapombe.

"Tunaendelea na mazoezi, dabi ni mechi ya kawaida kama nyingine, tatizo linakuja tu pale majina ya timu zinazocheza ni Simba na Yanga, labda hii ni kwangu kwa sababu nimeshacheza sana mechi hizi, binafsi sina presha, hata nikiamshwa usingizini naenda kucheza," aliongeza kiungo huyo.

Mkude ambaye alipandishwa kutoka katika kikosi cha U-20 na kuanza kucheza Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2011/2012, alitaja mchezo wake anaoukumbuka zaidi akiwa Simba ni ule ya raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika uliochezwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, dhidi ya Nkana Red Devils ya Zambia, Simba iliposhinda mabao 3-1 na kufuzu hatua ya makundi baada ya miaka mingi kupita.

"Ule ndiyo mchezo wangu bora ambao sitousahau kwa sababu tulifungwa mabao 2-1 ugenini, halafu tayari tulikuwa tumetanguliwa kwa bao moja nyumbani, lakini bao langu la kusawazisha liliturudisha mchezoni na kufanikiwa kufunga mawili mengine yaliyotupeleka hatua ya makundi.

Amemtaja nyota aliyekuwa anamhusudu na kuiga ubora wake ambao umechangia kufika hapo alipo ni kiungo wa zamani wa Simba, Mwinyi Kazimoto huku kwa sasa anavutiwa na Kelvin Nashon, ambaye anaichezea, Singida Black Stars.