STRAIKA wa zamani wa Yanga, Makumbi Juma, amesema moja ya sababu ambayo imeifanya timu hiyo kupoteza michezo miwili mfululizo katika mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara ni kucheza 'kifaza' kwa siku za karibuni, tofauti ya ilivyozoeleka huko nyuma.
Makumbi, ambaye alitisha kwa kupachika mabao akiwa na timu hiyo pamoja na timu ya taifa ya Tanzania kiasi cha mashabiki wa Yanga kumpachika jina la 'Homa ya Jiji', alisema msimu huu wachezaji wa timu hiyo wamebadilika na hawachezi kwa kujituma tena huku wakionekana kuridhika na mafanikio waliyoyapata huko nyuma.
"Nilichokigundua kwa siku za karibuni wachezaji wetu wanacheza kistaa sana, wanacheza 'kifaza', maana yake wao tayari ni wakubwa, wamekuwa maarufu, hivyo hawajitumi tena kwa sababu kila mmoja anafahamu wao ni nani, hiki kitu si kizuri, wabadilike," alisema Makumbi.
Aliwataka viongozi wa timu hiyo haraka wakae na Kocha Mkuu Miguel Gamondi ili awaambie wachezaji kuhusu mabadiliko ya uchezaji katika kikosi chao.
"Ningependa viongozi wakae na mwalimu awaambie kuhusu uchezaji wao na nidhamu yao. Siku hizi Yanga ikicheza na timu ambayo ina kasi, wanapambana na wana fiziki vizuri basi mechi kwao inakuwa ngumu sana tofauti na misimu miwili iliyopita, umeona mechi dhidi ya Tabora United na hata Singida Black Stars japo tulishinda bao 1-0," alisema.
Straika huyo mkongwe aliwataka viongozi wa klabu hiyo kuacha mpango wa kumtimua kocha Gamondi kama upo kwani haoni kama yeye ni sababu, badala yake kuna mambo kidogo tu ya kubadilika. "Sidhani kama ni sahihi kumtimua kocha kwa kufungwa, timu nyingi zinafungwa na hakuna timu isiyofungwa duniani," alisema.
Kuhusu kocha huyo kupenda kutumia wachezaji hao hao badala ya kubadilisha kitu ambacho kimemfanya kulaumiwa na baadhi ya wachambuzi, Makumbi alisema inawezekana kuna wachezaji wana mikataba migumu inayowataka kucheza kila mechi.
"Wachezaji wa sasa tofauti na sisi wa zamani, wanalipwa pesa nyingi na mikataba ina vipengele vingi, kuna baadhi wanaweza kuweka kipengele cha kucheza kila mechi ndiyo maana unaona kila mechi wapo, wengine ikitokea penalti anapiga yeye, imo kwenye mkataba, inawezekana kabisa kosa siyo la kocha, ni mikataba ya wachezaji," alisema.
Tangu kupoteza mechi mbili mfululizi, ikifungwa bao 1-0 dhidi ya Azam FC na mabao 3-1 dhidi ya Tabora United, hali imekuwa si tulivu sana kwenye klabu ya Yanga huku baadhi wakimnyooshea kidole Gamondi, lakini wengine lawama wakizitupa kwa baadhi ya wachezaji wa timu hiyo kwa kile kinachodaiwa kushuka viwango.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED