Meena, Masele waitwa Twiga Stars

By Somoe Ng'itu , Nipashe
Published at 12:55 PM Jul 01 2024
Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Clifford Ndimbo.
Picha: Mtandao
Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Clifford Ndimbo.

KOCHA Mkuu wa Timu ya Taifa ya Wanawake (Twiga Stars), Bakari Shime, amewaita kwa mara ya kwanza katika kikosi hicho, Victoria Masele anayecheza TopHat Soccer Academy ya Georgia na Malaika Meena wa Forest University ya Marekani, imeelezwa.

Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Clifford Ndimbo, alisema jana wachezaji hao wameitwa kwa ajili ya mechi za kirafiki za kimataifa dhidi ya Tunisia na Botswana zitakazofanyika hivi karibuni.

Ndimbo alisema wachezaji hao watawasili nchini hivi karibuni ili kuungana na nyota wengine wa timu hiyo watakaoingia kambini leo jijini Dar es Salaam.

"Kocha Shime amewaita wachezaji hawa ili kuongeza nguvu katika kikosi chake kwa sababu huko mbele tunahitaji kupata matokeo chanya kwenye mashindano yote ya kimataifa tutakayoshiriki," Ndimbo alisema.

Aliwataja wachezaji wengine walioitwa kuwa ni pamoja na Najat Abasi kutoka JKT,  Asha Mrisho ( Amani), Lidya Maximilian (JKT), Protasia Mbunda (Fountain Gate), Enekia Kasonga (Eastern Flames), Julietha Singano (Mexico), 

Vailet Mwamakamba ( Simba Queens), Anastazia Katunzi, Joyce Lema, Janeth Christopher (JKT), Ester Maseke (Bunda) na Diana Lucas wa Ame SKF.

Wachezaji wengine ni Aisha Juma (Simba Queens), Stumai Athumani, Winifrida Gerald (JKT), Maimuna Kaimu (ZED ya Misri),  Elizabeth Charles ( Alliance), Aisha Masaka (BK- Hacken), Oppa Clement (Besiktas) na Clara Luvanga anayecheza Saudi Arabia katika Klabu ya Al Nasr.

Twiga Stars imefuzu kushiriki fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wanawake (WAFCON), ambayo yamesogezwa mbele na Shirikisho la Soka Afrika (CAF), hadi Julai mwakani.