Ligi Kuu Zanzibar kurindima kesho

By Hawa Abdallah , Nipashe
Published at 05:14 PM Apr 26 2024
Mpira uliopigwa golini.
Picha: Mtandaoni
Mpira uliopigwa golini.

LIGI Kuu ya Zanzibar inatarajiwa kuendelea tena Aprili 28 mwaka huu baada ya kusimama kwa muda wa mwezi mmoja na nusu.

Ligi hiyo ambayo wakati inasimama tayari timu zote zilikuwa zimecheza michezo 20 ambapo iliyobaki ni michezo 10 ya kumaliza msimu wa Ligi wa 2023-2024.

Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Bodi ya Ligi Zanzibar inaonesha katika kisiwa cha Unguja kutakuwa na mchezo kati ya Zimamoto na Uhamiaji, mchezo ambao utachezwa katika uwanja wa Mao Zedong A siku hiyo ya Aprili 28.

Aidha mchezo mwingine ambao utachezwa katika uwanja wa Finya kisiwani Pemba utakuwa ni kati ya wakongwe wa soka visiwani hapa timu ya Jamhuri itakayopepetana na Hard Rock.

Hata hivyo, ratiba hiyo inaonesha siku ya pili ambayo itakuwa ni Jumatatu ya April 29, mwaka huu, pia kutakuwa na michezo miwili, ambapo Manedelo na Chipukizi watacheza uwanja wa Finya na Malindi itacheza na Mlandege Mao Zedong A.

Akizungumza na gazeti hili Mtendaji Kuu wa Bodi ya Ligi Zanzibar, Issa Kassim alisema maandalizi ya kuelekea michezo hiyo ya lala salama imekamilika.

Alisema Bodi ya Ligi kwa kushirikiana na kamati nyingine zinazohusika katika kusimamia Ligi hiyo watakuwa makini hasa katika michezo hii ya kupata  Bingwa na timu zinazoshuka daraja.

“Tunataka kuhakikisha hakuna vitendo vyoyote au viashiria vya upangaji wa matokeo katika michezo hii muhimu,”alisema.

Ligi kuu ya Zanzibar wakati inasimama ilikuwa ikiongozwa na timu ya Jeshi la Kujenga Uchumi (JKU), wenye alama 41, wakifuatiwa na mabingwa watetezi wa ligi hiyo KMKM wenye alama 39, wakati Zimamoto ipo nafasi ya tatu alama 37.

Jumla ya timu nne zinatarajiwa kushuka katika ligi hiyo, ambayo inashirikisha timu 16 katika msimu huu.