Kufuzu AFCON 2025 kwetu ni deni - Stars

By Somoe Ng'itu , Nipashe
Published at 11:32 AM Oct 11 2024
   Kufuzu AFCON 2025  kwetu ni deni - Stars
Picha:Mtandao
Kufuzu AFCON 2025 kwetu ni deni - Stars

WAKATI jana usiku ilishuka kuvaana na wenyeji DR Congo katika mechi ya Kundi H, Nahodha Msaidizi wa Timu ya Taifa (Taifa Stars), Mohamed Hussein 'Zimbwe Jr', amesema wachezaji wanafahamu wana 'deni' la kupambana kuhakikisha wanapata tiketi ya kushiriki Fainali zijazo za Kombe la Mataifa Afrika (AFCON 2025).

Taifa Stars itarudiana na DR Congo Oktoba 15, mwaka huu kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Akizungumza kabla ya kushuka dimbani jana, Zimbwe Jr, alisema kila mchezaji ambaye yuko katika kikosi hicho anajua kiu ya Watanzania ni kuona wanapata tiketi ya kushiriki fainali hizo za Afrika.

Beki huyo alisema ushirikiano wanaopata kutoka kwa serikali na wadau wa soka nchini, unawaongezea nguvu ya kupambana na kuhakikisha wanafikia malengo.

Naye Kaimu Kocha Mkuu wa timu hiyo, Hemed Morocco, alisema kikosi chake kinaendelea kuimarika na watacheza mechi zote, wanacheza bila presha yoyote.

Morocco alisema wanamheshimu kila mpinzani wanayekutana naye na wanajua kila timu inaposhuka uwanjani ina malengo ya kuondoka na pointi tatu.

"Tunaendelea kuimarika kadri tunavyoendelea kucheza mechi, tunapokuwa nje hatuna presha, tunapigana kuhakikisha tunapata matokeo, na nyumbani tunacheza bila presha. Watanzania waendelee kutusapoti, wana kiu ya kuona timu yao inafanya vizuri.

Kwa niaba ya wachezaji tunamshukuru Mama yetu Dk. Samia Suluhu Hassan amekuwa mdau mkubwa, Mtanzania namba moja, ni kitu cha faraja, ametupa ndege, amefanya mengi, na sisi kwa nafasi yetu tunatakia kusaka ushindi," alisema kocha huyo.

Mechi nyingine ya Kundi H inatarajia kuchezwa kesho kati ya wenyeji Guinea dhidi ya Ethiopia na timu hizo zitarudiana  keshokutwa kwenye Uwanja wa Abebe Bikila ulioko Addis Ababa.