Kamati yawakingia kifua waamuzi

By Faustine Feliciane , Nipashe
Published at 07:52 AM Oct 02 2024
MWENYEKITI wa Kamati ya Waamuzi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Nassoro Hamduni.
Picha: TFF
MWENYEKITI wa Kamati ya Waamuzi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Nassoro Hamduni.

MWENYEKITI wa Kamati ya Waamuzi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Nassoro Hamduni, amesema licha ya hivi karibuni kuibuka malalamiko juu ya waamuzi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, lakini kamati hiyo inaridhishwa kwa namna waamuzi hao wanavyofuata sheria zote za soka na adhabu wanazozitoa.

Baada ya mzunguko wa tatu wa Ligi Kuu, kumeibuka malalamiko kutoka kwa baadhi ya wadau wa soka juu ya maamuzi yanayotolewa na marefarii kwenye baadhi ya mechi.

Akizungumza jijini Dar es Salaam, Hamduni alisema kimsingi kamati yake haijapokea malalamiko yoyote licha ya kukiri kusikia kwa mashabiki.

"Hatujapata malalamiko yoyote rasmi, kama kamati tunaona kila kitu kinaenda vizuri, mwamuzi ni mwanamichezo na anaendeshwa na kanuni za ligi, anapokosea anaadhibiwa na kamati ya waamuzi adharani na watu wanajua," alisema Hamduni.

Alisema kwa sasa yanayosikika ni malalamiko tu ambayo hawawezi kuyazuia ila Kamati inaridishwa na mambo yanavyoenda sawa mpaka sasa kufikia raundi sita zilizochezwa. 

"Nawapongeza sana waamuzi kwa sababu wamechezesha vizuri na wanatoa adhabu pale inapostahili kulingana na kosa husika na kanuni zake," alisema.

Aliongezea kuwa kamati hiyo bado inaendelea kuwasisitiza waamuzi waendelee kuchezesha soka kwa kufuata sheria 17 kama wanavyofanya sasa.

Hivi karibuni kuliibuka malalamiko ya mashabiki baada ya mchezo kati ya Simba dhidi ya Dodoma Jiji ambapo baadhi walilalamikia adhabu ya penalti iliyotolewa kwa Simba na kuwapatia bao pekee kwenye mchezo huo.

Pia kulikuwa na malalamiko kwenye mchezo kati ya Yanga dhidi ya KenGold ambapo mwamuzi alilalamikiwa kwa kuwanyima goli KenGold.