Gamondi atamba kuonesha ukubwa

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 07:45 AM Sep 14 2024
Kocha Miguel Gamondi
Picha: Mtandao
Kocha Miguel Gamondi

MABINGWA wa Tanzania Bara, Yanga, leo saa 9:00 alasiri kwa saa za Tanzania wanarajiwa kushuka kwenye Uwanja wa Abebe Bikila, Addis Ababa, nchini Ethiopia kucheza na mabigwa wa nchi hiyo CBE katika mchezo wa mkondo wa kwanza, raundi ya kwanza Ligi ya Mabingwa Afrika, huku Kocha Miguel Gamondi akiahidi kuonesha ukubwa wao, licha ya kukiri kuwa hautokuwa mchezo rahisi kama wengi wanavyodhani.

Akizungumza kutoka nchini humo, Gamondi amesema CBE, inayomilikiwa na Benki ya taifa ya nchi hiyo, ni ngumu na ni mabingwa wa Ethiopia hivyo anatarajia mchezo mgumu ingawa ni lazima Yanga waoneshe ukubwa wao.

"Katika mchezo wa leo tunawaheshimu wapinzani wetu, tupo ugenini, lakini kwa timu kubwa kama Yanga tunatakiwa kuonesha ukubwa wetu, tuwe na nguvu ya kukabiliana nao," alisema kocha huyo raia wa Argentina.

Alisema amekuwa akiwasikia watu wakiibeza timu hiyo na kudhani mechi itakuwa rahisi kwa timu yake, lakini haitokuwa hivyo, na ndiyo maana amewaandaa wachezaji wake kukabiliana na mchezo mgumu.

"Siyo mechi rahisi na hasa ukicheza michuano ya kimataifa, kila timu ni ngumu, ina kiwango kikubwa na ni mabingwa kwenye nchi yao, lakini tunataka kufanya kila njia ili kuwadhibiti wapinzani wetu kwenye mchezo wa kwanza. Nataka tusipoteze, tupate matokeo mawili, ushindi au sare ili iwe mechi rahisi nyumbani," alisema kocha huyo ambaye msimu uliopita aliifikisha timu hiyo hatua ya robo fainali.

Gamondi alisema hakupata chochote cha kumsaidia kwa wachezaji wa CBE ambao walikuwa kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Ethiopia kilichocheza dhidi ya timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Septemba 4, hivyo maandalizi yake yametokana na taarifa za mchezo ambazo timu hiyo ilicheza dhidi ya SC Villa ya Uganda.

"Sikupata kitu chochote ambacho kinaweza kunisaidia kuwasoma wapinzani, kwa sababu wachezaji wao wanne wote hawakucheza, walikaa benchi tu, na pia hata kama wangecheza mfumo wa uchezaji wao timu ya taifa ungekuwa si sawa na wanapocheza kwenye kikosi cha CBE, hivyo isingenisaidia sana," alisema Gamondi.

Yanga ilitinga raundi ya kwanza ikishinda mabao 10-0 dhidi ya Vital'O ya Burundi, ikishinda mabao 4-0 mchezo wa kwanza na 6-0 mchezo wa pili, michezo yote ikipigwa, Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.

CBE ilifanikiwa kutinga hatua hiyo kwa kuifunga SC Villa nchini Uganda mabao 2-1 na kutoka sare ya bao 1-1 nyumbani.

Baada ya mechi ya leo, mchezo wa marudiano unatarajiwa kuchezwa Septemba 20 na mshindi wa jumla atatinga hatua ya makundi ya ligi hiyo.