Usimamizi ghala la pembe za ndovu umulikwe

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 06:31 AM Sep 22 2024
Pembe za ndovu.
Picha:Mtandao
Pembe za ndovu.

FEBRUARI 28, 2024, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa aliagiza Jeshi la Polisi kumkamata Mkuu wa Kitengo cha Fedha na Uhasibu wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti, mkoani Mara, anayetuhumiwa kushiriki uchepushaji fedha za umma zaidi ya Sh. milioni 213.

Akiwa ziarani wilayani Serengeti siku hiyo, Waziri Mkuu Majaliwa aliwataja wahusika wa uchepushaji huo, ambao alisema wanashirikiana na watumishi wengine watatu kutoka Kitengo cha Treasury Single Account (TSA) cha Ofisi ya Rais - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI).

Majaliwa aliutaja ni mtandao wa hujuma dhidi ya fedha za umma ambao si tu umebainika wilayani Serengeti, bali pia uko katika maeneo mengine nchini, ikiwamo mkoani Kigoma ambako nako alishabaini shida hiyo katika ziara zake zilizotangulia.

Kwa mujibu wa Majaliwa, wahusika wa wizi huo wa fedha za umma, wanafikia hadi kusafirisha fedha hizo kwa mabasi, wakiweka mamilioni ya shilingi katika mabegi ya nguo.

Wakati umma ukisubiri kuona hatua zinazochukuliwa dhidi ya watumishi hao, wakiwamo hao wanaotoka ofisi nyeti - Ofisi ya Rais, baadhi wakiwa wameshafikishwa mahakamani na kufunguliwa kesi za uhujumu uchumi na utakatishaji fedha, kuna dosari nyingine katika usimamizi wa ghala la pembe za ndovu nchini.

Kulikoni? Katika ripoti yake ya ukaguzi kwa mwaka 2021/22, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ameangazia suala hilo, akipendekeza Wizara ya Maliasili na Utalii kuweka mfumo madhubuti wa kusimamia pembe za ndovu nchini. 

CAG pia anapendekeza wizara iandae mfumo madhubuti wa taarifa zote zinazohusiana na pembe za ndovu, ukiwamo mpango mkakati wa taarifa za upotevu kutokana na matukio yasiyotarajiwa kama vile moto.

Shida ni nini? CAG anasema kuwa wakati wa ukaguzi wa hesabu za Wizara ya Maliasili na Utalii, amebaini kuwa Mei 16, 2022, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, aliunda timu ya uhakiki wa mali ambayo ilijumuisha wajumbe kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori nchini (TAWA), DW, Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro (NCAA) na Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA).

Anasema timu hiyo iliundwa kwa lengo la kuanzisha mchakato wa kuhesabu na kupima akiba ya nyara katika ghala la pembe za ndovu, jijini Dar es Salaam.

CAG anasema alibaini, pamoja na mengine, kutopatikana taarifa sahihi za pembe za ndovu zilizohifadhiwa kwa ajili ya kufanya tathmini na kuzipima upya pembe hizo.

Anasema pia alibaini hali isiyoridhisha ya pembe zote zilizohifadhiwa kiasi cha kusababisha kuharibika ubora na hadhi yake.

"Kwa maoni yangu, ukosefu wa udhibiti sahihi wa pembe za ndovu unaweza kusababisha upotevu wa taarifa zinazohusiana na pembe hizo,"

CAG alibaini shida nyingine ya kushindwa kuhuisha rejista juu ya hali na thamani ya pembe za ndovu, programu iliyotumika kurekodi na kusajili akiba ya pembe za ndovu na nyara zingine kutounganishwa na seva kuu ya programu ya wizara kwa sababu programu hiyo ilikuwa imepitwa na wakati.

CAG anasema katika ripoti yake kuwa, baadhi ya pembe za ndovu zilikosa taarifa zake za maandishi huku zingine zikiwa na taarifa zisizosomeka kutokana na ubovu wa paa la kuhifadhia, jambo linalosababisha kuvuja kwa paa hilo.

Anaongeza kuwa amebaini pia zana za kuwekea alama zilizotumiwa kurekodi taarifa kuhusu pembe za ndovu, ziliandikwa kwa wino unaoweza kufutika, hivyo kuzifanya ziweze kufutika kwa urahisi.

CAG anasema kuwa wakati wa ukaguzi, ghala la kuhifadhia nyara hizo lilikuwa katika hali mbaya kutokana na kuwa na nafasi ndogo, paa kuvuja, hewa chafu, mazingira machafu, umeme usio imara, ukosefu wa kamera na vifaa vya kuzima moto.

CAG anasema kuwa mbali na hayo, pia amebaini kuwa mwaka 2013, kulikuwa na tukio la moto katika ghala la pembe za ndovu ambalo lilisababisha kupotea kwa taarifa muhimu zinazohusiana na pembe za ndovu zilizohifadhiwa.

CAG anasema ni jambo la kushangaza kuwa hakuna uchunguzi uliofanyika ili kubaini chanzo cha moto huo na madhara yake hadi wakati wa ukaguzi wake.

"Kwa maoni yangu, ukosefu wa udhibiti sahihi wa pembe za ndovu unaweza kusababisha upotevu wa taarifa zinazohusiana na pembe hizo," anahadharisha. 

CAG anasema taarifa kuhusu pembe za ndovu ni muhimu katika kesi za kisheria dhidi ya ujangili na juhudi zingine zinazolenga kudhibiti vitendo vya ujangili.

Vilevile, CAG anabainisha kuwa Menejimenti ya Wizara ya Maliasili na Utalii imethibitisha kuwapo upungufu huo huku ikiahidi kufanya uhakiki wa nyara kila baada ya miaka mitatu hadi minne, kulingana na upatikanaji wa rasilimali.

Kwa mtazamo wangu, haya yaliyobainishwa na CAG yanapaswa kufanyiwa kazi, ikizingatiwa nchi bado inakabiliwa na changamoto ya ujangili, hasa wa tembo na faru ambao kuna kipindi waliripotiwa kuwa hatarini kutoweka nchini.

Vilevile, hoja hiyo ya CAG inapaswa kufanyiwa kazi kikamilifu, ikizingatiwa Sekta ya Utalii ni tegemeo katika kuingiza fedha zote za kigeni nchini, ikiajiri watu 600,000 ofisini na wengine zaidi ya milioni mbili iliowapa ajira zisizo za moja kwa moja. Sekta hii pia iliingiza Sh. trilioni 8.575 nchini mwaka 2022/23.

Kwa msingi huo, ujangili ukifumbiwa macho, pia kuwapo udanganyifu katika ghala la kuhifadhi nyara hizo za serikali, kutahatarisha uhai wa wanyamapori wanaolengwa zaidi na majangili, hasa ndovu na faru, hivyo kuweka rehani uchumi wa nchi.