DC,Meya wawafunda vijana Temeke wataka waachane na uchawa

By Pilly Kigome , Nipashe
Published at 08:03 AM Sep 22 2024
Meya wa Temeke, Abdallah Mtinika
Picha:Mpigapicha Wetu
Meya wa Temeke, Abdallah Mtinika

VIJANA wametakiwa kujitambue katika kuchagua na kupitisha viongozi wenye sifa katika uchaguzi ujao wa Serikali za Mitaa kwani wao ni hazina kubwa la kulipeleka mbele Taifa.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa Wilaya ya Temeke Sixtus Mapunda alipokuwa akizungumza katika Baraza la Vijana la Wilaya ya Temeke lililofanyika jijini Dar esSalaam.

Mapunda amewataka vijana hao kuwa wa kweli katika maamuzi na wasikubali kutumika vibaya kwa kupokea rushwa kwa kurubuniwa kupitisha viongozi ambao hawana sifa.

Naye Meya wa Temeke, Abdallah Mtinika amewataka vijana wajitambue, wajiheshimu, wajiamini ili waweze kutengeneza na kusimamia ndoto zao za uongozi katika safari za siasa.

“Kijana usikubali utumike kiholela, usikubali kutumika kama chawa ukajisahau kutengeneza ndoto zako, maisha ya sasa yamekaa kama filamu, penda watu wote, heshimu watu wote ufike safari yako, na mjitokeze kugombea nafasi zilizopo katika uchaguzi ujao, msiogope kugombea nafasi” amesema Mtinika

Kwa upande wake Katibu wa UVCCM Wilaya ya Temeke, Sayi Samba amesema wako katika kuwatengenezea vijana uwezo kwa kuwaandaa viongozi bora na makini wanaojitambua na kuhakikisha watashinda katika chaguzi katika mitaa yote 142 na kata 23 za Wilaya hiyo.

Aidha aliwataka vijana waachane na kauli za uzushi alizowahi kutoa kiongozi mmoja upande wa upinzani kuwa Rais Samia Sluhu Hassan atoke madarakani kuwa wapuuze kauli hiyo kwani nchi kwa sasa inaongozwa na Falsafa ya 4R ambazo Rais Samia Suluhu Hassan anazisimamia vyema.

3