Polisi yataja mambo matatu chanzo cha mauaji Dodoma

By Renatha Msungu , Nipashe
Published at 06:01 AM Sep 22 2024
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, George Katabazi
Picha: Mtandao
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, George Katabazi

JESHI la Polisi limebaini chanzo cha mauaji yaliyotikisa Jiji la Dodoma, likieleza kuwa kuna shida kuu tatu.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, George Katabazi, amesema mauaji hayo yalisababishwa na kisasi, wivu wa mapenzi na imani za ushirikina.

Amesema kuwa katika ufuatiliaji wa jeshi hilo, tayari watu wanane wamekamatwa na wengine watatu wameshafikishwa mahakamani kwa mashtaka ya mauaji. 

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini hapa, Kamanda Katabazi alisema kuwa kutokana na hali hiyo, moja ya mikakati waliyoweka ni kuhakikisha wanashirikiana na wananchi kuwakamata wahalifu kwa kuanzisha vikundi vya ulinzi shirikishi.

"Jeshi la Polisi limejipanga kukabiliana na matukio ya uhalifu mkoani hapa, Wanahabari waendelee kuhabarisha kile kinachofanywa na jeshi.

"Matukio haya yamekuwa mengi, lakini Jeshi la Polisi litahakikisha linakabiliana na wahalifu wa aina hii ili kutokomeza uhalifu unaojitokeza," alisema.

Kamanda huyo aliwaomba wananchi wasiogope kwenda kutoa taarifa polisi pale wanapoona kuna vitu hawavielewi katika mitaa mbalimbali wanamoishi na kusisitiza kwamba hakuna polisi atakayetoa siri za watoa taarifa.

Katika hatua nyingine, Kamanda Katabazi alisema wamekamata watu wawili wanaotuhumiwa kutengeneza noti bandia za Sh. 10,000 kwa ajili ya matumizi mbalimbali.

Alisema jumla ya Sh. 520,000 zimekamatwa pamoja na mashine ya kutengeza fedha bandia, ambazo huzitumia kubambika watu au kununua bidhaa mbalimbali madukani.

Kamanda Katabasi aliwataka wafanyabiashara wawe makini pale wanapopokea fedha kutoka kwa wateja wanaokwenda katika maduka yao kupata huduma mbalimbali.