Samia aagiza ustawi wa jamii kujitegemea

By Godfrey Mushi , Nipashe
Published at 07:58 AM Sep 22 2024
Waziri wa Wizara hiyo, Dk.  Dorothy Gwajima
Picha:Mtandao
Waziri wa Wizara hiyo, Dk. Dorothy Gwajima

SERIKALI imesema ipo katika hatua za mwisho kuanzisha Idara ya Ustawi wa Jamii inayojitegemea chini ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Makundi Maalum ili kurahisisha na kuimarisha uratibu, usimamizi na utekelezaji wa afua za ustawi wa jamii nchini.

Taarifa za kuundwa kwa idara hiyo, ilitolewa jana na Waziri wa Wizara hiyo, Dk.  Dorothy Gwajima, wakati akifunga mkutano wa tatu wa mwaka wa maofisa ustawi wa jamii katika Manispaa ya Moshi, mkoani Kilimanjaro.

Waziri Dk. Gwajima, alisema lengo la kuanzisha Idara ya Ustawi wa Jamii itakayojitegemea, ni ongezeko la uhitaji wa huduma za ustawi wa jamii kisekta kunako hitaji taasisi madhubuti katika kusimamia na kuratibu utoaji wa huduma hizo katika jamii kupitia Taasisi za umma, binafsi na wananchi kwa ujumla.

Kwa mujibu wa Waziri huyo, hatua hiyo ni matokeo ya kukubaliwa kwa  wasilisho la mapendekezo ya Haki Jinai kwa Rais Samia Suluhu Hassan.

Pamoja na mambo mengine, alisema mpango huo kwa sasa unasubiri maelekezo ya muundo wa Idara hiyo kupitia Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma.

"Namshukuru sana, Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ambaye ni Ofisa Ustawi wa Jamii namba moja, kwa kutambua mchango wa kazi zenu na kuipa kipaumbele tasnia hata kubariki tuendelee kufanya mkutano huu kila mwaka, ili kupata nafasi ya kujifunza mambo mazuri kutoka kwa wenzetu 

...na kujadili namna ya kutatua changamoto za ukatili wa aina mbalimbali zinazoikumba jamii yetu kwa sasa pamoja na namna ya kuboresha mazingira ya kazi tunapotekeleza majukumu yetu."

Kadhalika, Waziri Dk. Gwajima, alisema elimu itakayotolewa na moafisa hao itasaidia jamii kuelewa mambo mbalimbali ya huduma za kiustawi hasa huduma za unasihi kwa watoto, wazazi/walezi, huduma za uchangamshi wa awali ya watoto wadogo na huduma ya afya ya akili na msaada wa Kisaikolojia na kijamii  kwa makundi yenye uhitaji.

Aidha, alisema familia ndio taasisi pekee ambayo ni nguzo muhimu katika malezi bora inayomuandaa mtoto kuwa mwanaume au mwanamke bora wa baadaye, na familia ndiyo mahali salama kwa watoto kukua na kufikia utimilifu wao.

"Familia zimekuwa zikikukumbwa na changamoto nyingi ikiwemo umaskini, migogoro ya ndoa na familia, malezi duni kwa watoto inayopelekea kukosekana kwa muunganiko na mahusiano hafifu kati ya wazazi au walezi na watoto wao, ambapo athari zake ni pamoja na watoto kukosa upendo wa wazazi au walezi.

Zaidi aliongeza, "Kuendelea kuwepo kwa  mila na desturi za kukaa kimya na kuficha taarifa za vitendo vya ukatili hasa vinavyotokea ndani ya familia imesababisha kuendelea kuwepo kwa vitendo vya ukatili na kukosekana huduma kwa wahanga hali inayosababisha  mmomonyoko wa maadili na tabia hatarishi kwa watoto."

Awali, Mwenyetiki wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii, Fatma Tawfiq, alisema anatambua kuwa Wataalam hao wamefanya tathimini ya mambo yote yanayotakiwa ili kuboresha utendaji kazi zao na kutatua changamoto zao, ambapo Kamati yake itaendelea kuishauri Serikali kuongeza Bajeti ili kuwawezesha Maafisa Ustawi wa Jamii kutekeleza majukumu yao kwa ufasaha.

Mkutano wa tatu wa mwaka wa maofisa ustawi wa jamii, uliotangjliwa na  kauli mbiu 'Tanzania Bila Ukatili Inawezekana, Imarisha Mahusiano Ndani ya Familia' umefanyika kwa siku tatu, kuanzia Septemba 18 hadi 20 mwaka huu.