Makonda ageukia manabii, mitume feki

By Godfrey Mushi , Nipashe
Published at 07:44 AM Sep 22 2024
MKUU wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda
Picha:Mtandao
MKUU wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda

MKUU wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda amesema Tanzania hivi sasa inao viongozi wengi wa dini, lakini si maarufu kwa neno la Mungu au uponyaji kama walivyofanya mitume.

Kutokana na ombwe hilo, kwake yeye kama Makonda, Mwana wa Mungu, anawatangaza ni maaskofu feki, wachungaji feki, manabii feki na mitume feki.

Akitoa salaam za serikali jana katika viwanja vya Kisongo, jijini Arusha wakati wa mkutano wa injili wa Mtume Boniface Mwamposa (Buldoza), Makonda alisema:

"Wana wa Mungu niwaambieni, ukimwona kiongozi wa dini mwenye jina lakini umaarufu wake hautokani na kazi ya mikono ya Kristo, hautokani na kazi za Mungu; jua huyo ni kiongozi wa dini feki.

"Nchi yetu sasa hivi ina viongozi wengi wa dini lakini si maarufu kwa neno la Mungu. Maarufu kweli si kwa kazi ya uponyaji kama wanavyofanya mitume. Hao mimi Makonda, Mwana wa Mungu, ninawatangaza ni maaskofu feki, ni wachungaji feki, ni manabii feki, ni mitume feki.

"Yaani hii kofia ya ukuu wa mkoa, kuna wakati mimi huwaza, ninasema 'eeh Mungu wangu eeh...! Sijui ningechomoka kidogo ningekaa huku nihangaike na neno? Na watu ni waoga! 

"Eti mimi leo hii, ukuu wa mkoa, kanipa Samia (Rais Samia Suluhu Hassan), eti kutwa ninamsifia Mbowe (Freeman-Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo -CHADEMA), si nitafukuzwa kazi jamani?" alihoji Makonda.

Katika mkutano huo wa Mwamposa, Makonda, alisema amepewa atoe salamu na salamu zenyewe ndizo hizo.

Makonda aliwaeleza mamia ya waumini waliojitokeza katika mkutano huo kwamba watu wasiseme ameenda kusema kwa Mwamposa kwa kuwa "yeye ana kifua".

"Ninaweza kuchanganya makamasi na machozi, ninapiga magoti kumlilia Mungu kwa sababu ya Tanzania. 

"Mimi ni zao la maombi na wala sioni aibu. Apostle (Nabii) ananifahamu nikiwa chuoni, na wengi walitegemea nitakuwa mchungaji. Nikasema aah, wengine tumeitwa tu, lakini tunampenda Mungu. Kwani nyie (ninyi) watu wa Arusha si mnamwona Mungu? Kwani kuna manyanyaso? Fanya kazi ya aliyekuita, nawe utabarikiwa," Makonda alisema.