'Wamshukuru Rais Samia kwa moyo wake, awapa mil. 85/-'

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 09:30 AM Sep 23 2024
Stephane Aziz akiungana na Price Dube (katikati), sambamba na Kennedy Musonda, kushangilia baada ya kuifungia timu yake moja kati ya mabao matatu (hat-trick), wakati wakishinda 6-0 dhidi ya CBE ya Ethiopia kwenye mechi ya marudiano ya raundi ya kwanza
Picha: Mtandao
Stephane Aziz akiungana na Price Dube (katikati), sambamba na Kennedy Musonda, kushangilia baada ya kuifungia timu yake moja kati ya mabao matatu (hat-trick), wakati wakishinda 6-0 dhidi ya CBE ya Ethiopia kwenye mechi ya marudiano ya raundi ya kwanza

KLABU ya Yanga, imeendelea kutembelea upepo mzuri wa kuvuna mamilioni ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, baada ya juzi usiku visiwani Zanzibar, kuifunga timu ya CBE ya nchini Ethiopia mabao 6-0, hivyo wawakilishi hao wa Tanzania kuvuna Sh. milioni 30 za rais, kama sehemu ya motisha ya ushindi wao.

Kwa ushindi huo, Yanga imefanikiwa kufuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu wa 2024/2025, ikiwa ni mwendelezo mzuri katika michuano ya Kimataifa kwa Yanga, ambapo pia kwenye mchezo wa kwanza uliochezwa Ethiopia, waliibuka na ushindi wa bao 1-0, hivyo kuvuna Sh. milioni tano 'Bao la Mama'.

Tangu Rais Samia aanzishe motisha wa Bao la Mama, Yanga wameonesha shauku kubwa ya kupata fedha hizo, ambapo kwa msimu huu tu tayari wamevuna Sh. milioni 85.

Katika raundi ya awali, Yanga ilishinda mabao 4-0 dhidi ya Vita'O na marudiano ikaibuka na ushindi wa mabao 5-0, hivyo kujikusanyia jumla ya Sh. milioni 50 kabla ya kuvuna Sh. milioni 35 kwa ushindi wa jumla wa mabao 7-0 walioupata dhidi ya CBE.

Akizungumza baada ya kukabidhiwa fedha hizo, Rais wa Yanga, Engineer Heris Said, alisema motisha wa Rais Samia unachangia kwa kiasi kikubwa timu yao kupata mafanikio makubwa katika michuano ya kimataifa.

Alisema tangu Rais Samia aanze kuonesha upendo kwa klabu za Tanzania, timu yao imekuwa ikitumia mwanya huo kuhakikisha kwamba wanatamba katika michuano ya kimataifa, wakiamini kuwa Bao la Mama ni maalum kwa kuwapa wachezaji wao moyo wa kufia uwanjani kama sehemu ya kukuza mchezo wa mpira wa miguu nchini Tanzania.

"Upendo huu ni mkubwa kwa rais wetu, hivyo tunamshukuru Mama Samia kwa kutuweka pazuri ndani na nje ya nchi, ndio maana tunashinda kwa magoli mengi uwanjani kwa sababu wachezaji wanafahamu shauku ya rais wetu ni kuona timu inashinda na kupata mafanikio makubwa.

"Hata ukiangalia wachezaji wanapokuwa uwanjani, utagundua nguvu zao nyingi zinachagizwa pia na mamilioni ya Rais Samia, kwetu Yanga tunamshukuru kwa kuonyesha upendo dhidi ya timu yetu," alisema Hersi.