Sanamu la Mwalimu Nyerere labomolewa, vipande vyaibwa

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 10:49 AM Sep 23 2024
Vipande vya  Sanamu la Mwalimu Nyerere lililovunjwa Mtaa wa Matola, Kata ya Chemchem Manispaa ya Tabora.
Picha:Mtandao
Vipande vya Sanamu la Mwalimu Nyerere lililovunjwa Mtaa wa Matola, Kata ya Chemchem Manispaa ya Tabora.

SANAMU la Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere lililoko Kata ya Chemchem, Manispaa ya Tabora limebomolewa na baadhi ya sehemu zake ikiwamo shingo, fimbo pamoja na kiganja kuibwa.

Tukio hilo lilifanywa usiku wa kuamkia Septemba 21, mwaka huu kwenye eneo hilo ambako wahusika hawajajulikana.

Ofisa Mtendaji wa Kata ya Chemchem, Salehe Mbuguma, alisema jana kuwa alipigiwa simu na watu asubuhi akielezwa kutokea kwa tukio hilo na kwamba walikuta sanamu liko chini, huku kichwa kikiwa kimefungwa kwenye kitambaa cheupe, kipande cha nguo ya rangi nyeusi na sarafu ya Sh. 200.

Mbuguma alisema sanamu hilo walilikuta likiwa chini na limevunjwa vipande vitatu ambavyo ni kichwa, kiwiliwili cha kuanzia shingoni hadi kiunoni na sehemu ya chini kuanzia kiunoni hadi miguuni na kwamba hawakukuta fimbo ya mfano wa aliyokuwa anashika Mwl. Nyerere.

Diwani wa Mpera, Manispaa ya Tabora, Haruna Msoga, alisema sanamu hilo lina uzito wa kilo 6,000 na lilitolewa jijini Arusha kwenda Tabora mwaka 1988 kwa ajili ya maadhimisho ya sherehe za Chama Cha Mapinduzi (CCM) kitaifa.

Msoga alisema kuwa wakati sanamu hilo linawekwa, eneo hilo lilipandishwa kwa mashine maalum na lilizinduliwa na Mwl. Nyerere.

"Tukio hili si la kiungwana na limetufedhehesha wana Tabora, sanamu hili liliwekwa maalum kwa ajili ya kumbukumbu ya Hayati Mwl. Nyerere, kuenzi harakati zake za kupambania uhuru wa nchi hii na hapa ndipo alipohutubia na kutokwa machozi baada ya kufanyika uamuzi wa busara wa kupigwa kura tatu za kung’oa mkoloni na kujipatia uhuru wetu," alisema.

Aliiomba serikali kufanya uchunguzi wa kina kubaini mwenendo wa tukio zima na kuwakamata wahusika sambamba na kuwachukulia hatua kali za kisheria.

Mkurugenzi wa Manispaa ya Tabora, Elias Kayandabila, alisema wako katika mchakato wa kuboresha eneo hilo ikiwa ni pamoja na kujenga majengo mapya kwa kuzingatia kuwa "eneo hilo ni nyeti".

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Kamishna Mwandamizi Richard Abwao alisema kuwa wanaendelea na uchunguzi wa tukio hilo kubaini uhalisia wa tukio hilo, kuwatafuta, kuwakamata na kuwafikisha katika vyombo vya kisheria wahusika watakaobainika.

"Tumefika eneo la tukio na kubaini kuwa limeondolewa katika eneo lake la mnara na kuvunjwa vipande vipande, hapa kikubwa tunachunguza ni mazingira gani yamesababisha sanamu hilo linafika chini," alisema Abwao.

Alisema katika uchunguzi wa awali walibaini baadhi ya vipande kutokuwapo na kuwa changamoto ni kuwa eneo hilo halina umeme, pia halikuwa na ulinzi wa aina yoyote.