Wafugaji waanzisha kijiji cha utalii

By Ashton Balaigwa , Nipashe
Published at 11:25 AM Sep 23 2024
Wafugaji waanzisha kijiji cha utalii
Picha: Mtandao
Wafugaji waanzisha kijiji cha utalii

WAFUGAJI wa kabila la Kimasai wametumia fursa ya kuwapo Hifadhi ya Taifa Mikumi (MINAPA) wilayani Kilosa, mkoani Morogoro kuanzisha Kijiji cha Utalii wa Kitamaduni wa kabila hilo walichokipa jina la "Mikumi Masai Boma".

Utalii huo wa kitamaduni unapatikana katika Kijiji cha Kikwalaza, Mikumi ambako watalii wanapata fursa ya kujifunza mambo mbalimbali ya kabila la Wamasai.

Akizungumza na Nipashe mwishoni mwa wiki, Mratibu wa Mikumi Masai Boma, Nuhu Mereni, alisema wameamua kuanzisha utalii huo ili kuwavutia zaidi wageni wanaotembelea Hifadhi ya Taifa ya Mikumi kujua utamaduni wa kabila hilo, ukijumuisha vyakula wanavyotumia.

Alisema watalii hao wanapofika katika Kijiji cha Utalii cha Mikumi Masai Boma, kwanza wanavalishwa mavazi ya kimasai, watapekechewa moto na kupewa historia ya kabila hilo pamoja na michezo mingine, ikiwamo ngoma.

Mratibu huyo wa Mikumi Masai Boma alisema kuwa, pamoja na mambo mengine, watalii hao watapata fursa ya kufundishwa kuchunga ng'ombe na kuoneshwa makazi ya kijadi ya kabila hilo.

"Tunashukuru kuwapo hifadhi hii ya Mikumi na sisi kama wafugaji wa kabila la Kimasai wa wilayani Kilosa, tukatumia fursa hiyo kuonesha utamaduni wetu ambao wageni wanaotembelea hifadhini, wamekuwa wanapendezwa nao na kuingiza mapato - fedha," alisema Nuhu.

Mwanzilishi wa Utalii wa Utamaduni nje ya Hifadhi ya Taifa Mikumi, Makene Ngoromo, alisema kuwa wameanzisha utalii mpya wa kitamaduni wa kabila la Wavidunda wanaoishi pembezoni mwa Hifadhi ya Taifa Mikumi na Udzungwa.

Alisema kupitia utalii huo wa Wavidunda, waliainisha vivutio mbalimbali, zikiwamo aina tano ya maporomoko ya maji ambayo yanapatikana katika Milima ya Wavidunda iliyoko katika Milima ya Tao la Mashariki.

Alisema kuwa katika milima hiyo pia wanaishi kabila hilo la Wavidunda ambao maisha yao yamekuwa kivutio pamoja na mazao yao ya kilimo katika milima hiyo ambayo ni kivutio kikubwa kwa watalii wengi.

Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Mikumi, Augustine Masesa, alisema hifadhi hiyo ni moja ya alama za uhifadhi zilizorithiwa toka kwa wazee, ikiwamo bayonuai na wanyamapori, hivyo imeona pia umuhimu wa kutoa fursa kwa utalii wa utamaduni wa makabila mbalimbali yanayozunguka eneo hili ili kuongeza kipato.