TBS yatoa hadhari ununuzi wa bidhaa pasipo kuhakiki

By Joseph Mwendapole , Nipashe
Published at 10:33 AM Sep 23 2024
Pichani Afisa Masoko (TBS) Deborah Haule, akitoa elimu ya viwango kwa mzalishaji wa bidhaa wakati wa Tamasha la Tisa la Biashara visiwani Zanzibar.
Picha: Maktaba
Pichani Afisa Masoko (TBS) Deborah Haule, akitoa elimu ya viwango kwa mzalishaji wa bidhaa wakati wa Tamasha la Tisa la Biashara visiwani Zanzibar.

SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS) limewataka wananchi kuhakikisha wanasoma kwa makini taarifa za vifungashio kwenye bidhaa kabla ya kufanya ununuzi.

Lengo ni kujiridhisha endapo bidhaa hizo zimethibitishwa ubora na hazijaisha muda wake wa matumizi pamoja na taarifa zingine za msingi kwa lengo la kulinda afya zao.

Ofisa Masoko wa shirika hilo, Deborah Haule  alitoa tahadhari hiyo wakati wa mwendelezo wa kampeni ya elimu kwa umma illiyotolewa mkoani Kigoma. Wananchi 2,730 pamoja na wajasiriamali 110 walifikiwa.

Alisema lengo la kampeni hiyo ni kuelimisha wananchi kuhusiana na umuhimu wa kutumia bidhaa zilizothibitishwa ubora, jinsi ya kutoa taarifa za bidhaa hafifu pamoja na zile ambazo hazijaisha muda wake wa matumizi.

Alisema kupitia kampeni hiyo, serikali kwa kutambua mchango wa wajasiriamali katika kukuza uchumi wa nchi na uchumi wao binafsi inathibitisha ubora wa bidhaa wanazozalisha bure.

Deborah alisema mashirika ya viwango ya nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) yameingia makubaliano, kwamba bidhaa ikishapimwa na kuthibitishwa na shirika la viwango la nchi husika, ikivuka mipaka na kwenda nchi nyingine haitakiwi kupimwa tena.

"Kwahiyo, hii ni fursa nzuri kwa wajasiriamali wanaothibitisha bidhaa zao wanachotakiwa ni kuja na barua ya utambulisho kutoka Shirika la Viwanda Vidogo (SIDO) hatutaki kumwacha nyuma mjasiriamali yeyote," alisema.

Alisema TBS inatoa elimu hiyo kwa lengo la kuwajengea wananchi uelewa kuhusu umuhimu wa viwango ili kulinda afya za walaji na kuwawezesha wazalishaji bidhaa kihimili soko la ndani na nje ya nchi.

Alisema matakwa ya ubora ni pamoja na bidhaa kuwa na tarehe ya mwisho wa matumizi, hivyo kupitia kampeni hiyo wanaelimisha jamii na  wadau kuhusu taarifa za kuzingatia kwenye vifungashio kabla ya kununua bidhaa.

Deborah alisema elimu hiyo inatolewa kwa wananchi kupitia maeneo ya wazi, ikiwamo minadani, vituo vya mabasi, masoko na maeneo mengine yenye mikusanyiko ya watu wengi.

Ofisa Udhibiti Ubora wa TBS, Peter Musiba, aliwataka wafanyabiashara kujitokeza kusajili vyakula na vipodozi ili kuwawezesha kufanya shughuli zao kwa kukidhi matakwa ya sheria za nchi na kulinda afya za walaji.