Job: Fedha za Mama zinatupandisha morali

By Faustine Feliciane , Nipashe
Published at 09:35 AM Sep 23 2024
Beki wa kati wa Klabu ya Yanga, Dikson Job.
Picha: Mtandao
Beki wa kati wa Klabu ya Yanga, Dikson Job.

BEKI wa kati wa Klabu ya Yanga, Dikson Job, amesema ushindi mkubwa wanaoupata kwenye michuano ya kimataifa unachangiwa kwa kiasi kikubwa na ahadi ya fedha za Rais Samia Suluhu Hassan anazozitoa kwa kila bao wanalofunga.

Job ambaye kwenye mchezo wa juzi dhidi ya CBE ya Ethiopia alikuwa nahodha wa timu hiyo, alisema, kila wakati wamekuwa wakihamasishana wachezaji kupambana uwanjani kwa sababu ya fedha hizo na kuendelea kuwapa furaha Wanayanga.

“Ni kweli kabisa ushindi huu na hata mechi iliyopita kwenye michuano hii, pesa za mama yetu zimekuwa zikitupa hamasa sana, huwa zikitolewa tunagawana wachezaji wenyewe, kwa hiyo kila mmoja huwa anajitolea kuhakikisha tunapata ushindi mkubwa tupate pesa nyingi,” alisema Job.

Akizungumzia mchezo huo wa juzi, Job alisema ulikuwa mgumu kutokana na aina ya uchezaji wa wapinzani wao.

“Kipindi cha kwanza wapinzani wetu walikuwa wengi sana kwenye eneo lao la nyuma, walitoa upinzani wa namna ya kufika golini kwao na ndio maana uliona hatukupata magoli mengi, lakini tulipoenda mapumziko kocha alitupa maelekezo na tuliporejea tulianza kwa kasi na kufanikiwa kupata bao la mapema kipindi cha pili,” alisema Job.

Alisema baada ya bao hilo la pili waliendelea kuimarika kimchezo na kuwabana wapinzani wao kwenye eneo lao na kufanikiwa kupata mabao sita.

“Kwa sasa tumemaliza hatua hii, tunaelekea hatua ya makundi kocha wetu anajua nini tunatakiwa kufanya kuweza kufanya vizuri zaidi ya msimu uliopita,” alisema.

Aidha, alisema upana wa kikosi chao pia unachangia sana kupata matokeo mazuri kwenye michezo mingi.

“Kila mchezaji ana uwezo mkubwa, kila anayepata nafasi ya kucheza anaonesha kile ambacho mwalimu anataka, ukiangalia kwenye mchezo huu kuna wachezaji wa kikosi cha kwanza walikuwa nje, lakini waliopata nafasi ya kuanza waliendelea kufanya kile ambacho kocha wetu anakitaka, tuna kikosi kizuri,” alisema Job.

Kwenye mchezo huo ulioisha kwa ushindi wa mabao 6-0, Job alicheza beki wa kati pamoja na Ibrahim Bacca na kufanikiwa kuwadhibiti washambuliaji wa Rais Samia Suluhu.