Takwimu na rekodi 10 za mabao Ligi Kuu Kuu Bara

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 09:09 AM Sep 23 2024
news
Picha:Mtandao
Wachezaji wa Azam FC, wakishangilia moja ya mabao yao manne waliyofunga katika mchezo wao dhidi ya KMC , uliopigwa Uwanja wa KMC Complex, Mwenge, Dar es Salaam, Alhamisi iliyopita, ikiwa ni moja kati ya michezo miwili iliyotoa vipigo vikubwa kwenye Ligi

JUMLA ya mabao 53 yalikuwa yamefungwa kwenye michezo ya Ligi Kuu Tanzania Bara mpaka kufikia juzi, Jumamosi.

Mabao hayo yamefunga na wachezaji 40 katika michezo 30 ambayo imechezwa mpaka sasa. Tayari Ligi Kuu Tanzania Bara imeshaingia raundi ya tano kwa baadhi ya timu, lakini zingine bado hazijacheza hata raundi mbili, ikiwamo Yanga.

Kwenye makala haya, tunakuletea aina na staili ya mabao hayo 53 yaliyofungwa mpaka sasa, huku pia wakiwamo timu na wachezaji walioweka rekodi ya mabao hayo, twende sasa... 

1# Mabao matatu ndani ya sekunde chache

Jumla ya mabao matatu yamefungwa kabla dakika moja haijakamilika. Septemba 12, Paul Peter wa Dodoma Jiji alifunga bao sekunde ya 39, wakati timu yake ikiichapa Namungo bao 1-0, Uwanja wa Tanzanite Kwaraa, Septemba 17,  Emmanuel Keyekeh wa Singida Black Stars, naye alipachika mabao sekunde ya 20, likiwa ni bao pekee, timu yake ikiichapa Pamba Jiji 1-0, Uwanja wa CCM Kirumba Mwanza, na Septemba 20, mwaka huu, Peter Lwasa akiifungia Kagera Sugar bao sekunde ya 51, ikishinda nyumbani, Uwanja wa Kaitaba, Bukoba mkoani Kagera.     

2# Mabao 32 ya mguu wa kulia

Mabao 32 yamefungwa kwa mguu wa kulia mpaka sasa, huku Fountain Gate ikiongoza kwa wachezaji wake kupachika mabao kwa mguu huo.

Kati ya mabao tisa ambayo wamefunga mpaka sasa, manane yakifungwa kwa mguu wa kulia, wakifuatiwa na timu ya Simba na Singida Black Stars ambazo wachezaji wao wamefunga mabao sita kila moja kwa kutumia mguu huo. 

3# Mabao 14 ya mguu wa kushoto

Wakati mabao 14 yakiwa yamefungwa kwa mguu wa kushoto kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara mpaka sasa, Tabora United ndiyo inayoongoza kwa kupachika mabao mengi kwa kutumia mguu huo.

Wachezaji waliofanya hivyo mpaka sasa, ni Heritier Makambo, Shedrack Asiegbu na Yacouba Songne, ambao wameifanya kuwa na mabao matatu ya mguu wa kushoto, huku KMC ikifuatiwa ikiwa imepachika mabao mawili kwa kutumia mguu huo, kupitia kwa mchezaji wake Redemtus Mussa, aliyefunga mabao yote hayo. 

4# Mabao saba ya vichwa

Mabao saba yamefungwa kwa vichwa mpaka sasa, huku Simba na Singida Black Stars ndizo zinaongoza kila timu ikipachika mabao matatu kwa njia hiyo.

Straika wa Singida Black Stars, Elvis Rupia, anaongoza kwa kufunga mabao mawili peke yake kwa njia hiyo na kuwa mchezaji kinara kwenye Ligi Kuu mpaka sasa kufungwa kwa vichwa. Mchezaji mwingine wa Singida ni Mohamed Damaro.

Kwa upande wa Simba, Che Fondoh Malone, Edwin Balua na Valentine Mashaka, wamefunga mabao hayo kwa njia hiyo katika michezo miwili ambayo timu hiyo imecheza mpaka sasa. 

5# Mabao 44 ndani ya boksi

Kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara mpaka sasa jumla ya mabao 44 yamefungwa ndani ya eneo la hatari na wachezaji mbalimbali, huku wa Fountain Gate wakionekana makini sana wakiwa ndani ya boksi.

Timu hiyo imefunga mabao manane ambayo wachezaji wake wakiwa ndani ya boksi na kuwa timu inayoongoza kwa kufunga mabao wakiwa karibu na lango. 

6# Mabao tisa nje ya boksi

Yamefungwa mabao tisa nje ya eneo la hatari mpaka sasa, na KMC ndio wanaoongoza kwa kupachika mabao mawili wakiwa nje ya boksi.

Na aliyewafanya kuweka rekodi hiyo mpaka sasa ni mchezaji wao, Redemtus Mussa, ambaye amefunga mabao yote akiwa nje.

Kumbuka mchezaji huyu ndiyo aliyefunga mabao mawili kwa mguu wa kushoto, akiifanya timu yake kuwa ya pili, yote aliyafunga nje ya boksi. 

7# Mabao matano ya penalti

Kati ya mabao 53 yaliyofungwa, mabao matano yamefungwa kwa mikwaju ya penalti. Jumla ya penalti nane zimetolewa na waamuzi, lakini tano ndiyo zilizotinga nyavuni na tatu zikaota mbawa.

Wachezaji ambao wamepachika mabao kwa mikwaju ya penalti mpaka sasa ni Djuma Shaaban wa Namungo, Makambo na Asiegbu, wote wa Tabora United, Ibrahim Elias wa KMC na Salum Kihimbwa wa Fountain Gate. 

8# Bao moja la kujifunga

Kuna bao moja tu la kujifunga mpaka sasa, na lilipatikana Septemba 19, mwaka huu, Uwanja wa KMC Complex, Mwenge, Dar es Salaam, ambapo Fred Tangalo wa KMC aliuweka mwenyewe mpira wavuni katika harakati za kuokoa timu yake ilipocheza dhidi ya Azam FC na kupoteza kwa mabao 4-0. 

9# Mechi mbili za vipigo vikali

Ni michezo miwili tu ambayo imetoa vipigo vikali zaidi mpaka sasa. Michezo hiyo ni ile ambayo Simba iliichakaza Fountain Gate mabao 4-0, mchezo ukichezwa, Agosti 25, Uwanja wa KMC Complex, Mwenge, Dar es Salaam, na ule uliopigwa, Septemba 19, Azam ikiibamiza KMC mabao 4-0 kwenye uwanja huo huo. 

10# Mabao ya faulo

Mpaka sasa ni mabao mawili tu yaliyofungwa kwa faulo ya moja kwa moja. Wachezaji waliopachika mabao kwa njia hiyo ni Dickson Ambundo wa Fountain Gate na Redemtus wa KMC.

Ambundo alifanya hivyo, Septemba 15, akipopiga faulo iliyokwenda moja kwa moja wavuni, akiiandikia timu yake bao la pili la kusawazisha, Uwanja wa Tanzanite Kwaraa, Babati, Manyara, dhidi ya Dodoma jiji na kumalizika kwa sare ya 2-2, na kwenye Uwanja wa KMC Complex, Redemtus alifunga kwa mkwaju wa faulo na kuipatia bao pekee katika mchezo dhidi ya KenGold, Septemba 16, mwaka huu.