Simba SC yatinga makundi ilipozoea

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 09:15 AM Sep 23 2024
Kiungo mshambuliaji wa Simba, Kibu Denis, akimtoka beki wa kati wa Al Ahli Tripoli, Ahmed El Trbi, kwenye mechi ya marudiano ya hatua ya kwanza ya Kombe la Shirikisho Afrika iliyopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa
Picha:Mpigapicha Wetu
Kiungo mshambuliaji wa Simba, Kibu Denis, akimtoka beki wa kati wa Al Ahli Tripoli, Ahmed El Trbi, kwenye mechi ya marudiano ya hatua ya kwanza ya Kombe la Shirikisho Afrika iliyopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa

WAWAKILISHI wa Tanzania katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, Simba, wamefanikiwa kutinga hatua ya makundi ya michuano hiyo mara ya pili kwa kipindi cha misimu minne baada ya kuiadhibu Al Ahli Tripoli mabao 3-1 katika mchezo mkali na mgumu uliopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Yalikuwa ni mabao ya Kibu Denis, Leonel Ateba na Edwin Balua yaliyoipeleka Simba hatua hiyo ambapo sasa itasubiri droo inatayochezwa baadaye mwezi ujao.

Ulikuwa ni mchezo wa mkondo wa pili baada ya ule wa kwanza wa raundi ya kwanza Jumapili iliyopita kwenye Uwanja wa Juni 11, nchini Libya, timu hizo kutoka suluhu.

Hii inakuwa ni mara ya nane kwa Simba kucheza ligi za kimataifa, tangu zilipoanza kuchezwa kwa mtindo wa makundi, Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho.

Pia ni mara ya tatu mfululizo kutinga makundi ya mechi za kimataifa kwani misimu miwili iliyopita ilicheza hatua kama hizo za Ligi ya Mabingwa Afrika.

Haikuwa rahisi kwa Simba kutinga hatua hiyo, kwani ilipigana machozi, jasho na damu kuweza kupata mabao hayo, kutokana na kutangulia kufungwa.

Simba ilianza kugonga hodi langoni mwa wapinzani wao dakika ya pili tu, baada ya Shomari Kapombe kuambaa na mpira kwenye wingi ya kulia, lakini krosi aliyopiga ilishindwa kuzuiwa na Joshua Mutale na kusababisha mabeki waokoe.

Dakika nne baadaye ilirejea tena, safari hii krosi ya Mohamed Hussein 'Tshabalala', ilikwenda langoni, lakini Ateba aliyekuwa katika nafasi nzuri, akateleza na kuanguka, akiwapa fursa mabeki wa Al Ahli kuuokoa mpira huo.

Kosa lililofanywa na Tshabalala dakika ya 10 nusura liwapatie bao Al Ahli, kwani alirudisha fyongo langoni mpira kwa kichwa, lakini ulikuwa mfupi, shukrani kwa kipa Moussa Camara aliyeuwahi kabla ya straika hatari, Agostinho Cristovao Paciencia maarufu kama Mabululu hajaifikia.

Mabululu aliwashtua mashabiki wa Simba dakika ya 17 kwa kuukwamisha mpira ndani ya wavu, akitumia uzembe wa mabeki wa timu hiyo kushindwa kuokoa mpira wa faulo iliyopigwa na Sunday Masoud.

Faulo hiyo ilipigwa kwenye wingi ya kushoto, ukarudishwa ndani na Mohamed El Munir, mabeki wa Simba wakazubaa, mpira ukawekwa ndani ya wavu.

Simba ingeweza kusawazisha bao dakika tatu baadaye kama si shuti la Joshua Mutale lisingemgonga mmoja wa mabeki wa timu hiyo na kutoka nje.

Kibu aliisawazishia Simba bao dakika ya 35, kwa 'kutambuka' kwa ustadi na kuunganisha mpira wa kichwa uliopigwa na Fondoh Che Malone.

Ulikuwa ni mpira wa adhabu uliopigwa na Jean Charles Ahoua ambao ulipigwa kichwa na beki huyo ukarejea ndani kabla ya kumkuta mfungaji ambaye aliukwamisha wavuni licha ya kipa Ayman Al Tihar kujitahidi kuokoa.

Sekunde chache kabla ya kwenda mapumziko, Ateba aliwainua vitini mashabiki wa Simba alipopachika bao la pili baada ya kupokea pasi ya kupenyezwa kutoka kwa Mutale.

Yalikuwa ni makosa ya mmoja wa mabeki wa Al Ahli Tripoli kurudisha mpira nyuma, ambao uliporwa na wachezaji wa Simba na kufanya shambulio lililozaa bao hilo.

Kipindi cha pili kilikuwa na presha zaidi kwa wachezaji, viongozi, benchi la ufundi na mashabiki wa Simba kwani walihitaji bao moja ambalo lingewaweka salama, lakini haikuwa hivyo mapema.

Kila mmoja alitambulia kuwa kama wapinzani wangepata sare yoyote ile, wawakilishi hao wa Tanzania walikuwa wanasukumizwa nje ya michuano hiyo.

Ni kipindi ambacho kasi iliongezeka zaidi kuliko cha kwanza, huku Simba ikionekana kucheza nyuma ya mpira kwa muda mwingi wa mchezo.

Matukio ya kukumbukwa zaidi yalianza kutokea dakika moja kabla ya mechi kumalizika, wakati Al Ahli Tripoli walipokuwa wamehamia langoni mwa Simba, ambapo Mabululu aliachia mkwaju mkali ulioonekana unakwenda kutinga wavuni, lakini kwa ustadi wa kipa Camara, aliruka juu kama nyani na kuupangua mpira ukawa kona.

Kona hiyo ndiyo iliyokuwa kaburi lao, kwani wakati wanashambulia, Simba iliunasa na kufanya shambulizi la ghafla, kwa mpira mrefu ambao uliomkuta Balua, aliyekuwa ameingia kipindi cha pili, akakokota mpira kwa umbali mrefu, akawahadaa mabeki na kipa Ayman, kabla ya kuujaza wavuni kwa mguu wa kushoto.