Gamondi: Hakuna wa kumwogopa makundi

By Faustine Feliciane , Nipashe
Published at 09:21 AM Sep 23 2024
Kocha wa Yanga, Miguel Gamondi.
Picha:Mtandao
Kocha wa Yanga, Miguel Gamondi.

BAADA ya kuiwezesha timu yake kufuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Kocha wa Yanga, Miguel Gamondi, amesema kwa sasa hakuna timu wanayoihofia kukutana nayo kwenye hatua hiyo.

Yanga juzi usiku iliitoa CBE ya Ethiopia kwa jumla ya mabao 7-1 baada ya kushinda 6-0 katika Uwanja wa New Amaan Complex visiwani Zanzibar, ushindi huo ukija wiki moja baada ya kutoa kipigo cha bao 1-0 ugenini.

Akizungumza juzi baada ya mchezo huo wa marudiano hatua ya kwanza ya michuano hiyo, Gamondi, alisema wanachokifanya ni kuwaheshimu wapinzani wao, lakini hakuna timu wanayoihofia.

Gamondi, alisema kufuzu kwa Yanga kwenye hatua hiyo ni jambo jema kwa nchi kwani inakuwa mwakilishi kwenye michuano hiyo mikubwa kwa ngazi za Klabu Afrika.

“Sasa tunasubiri droo ya makundi, tunashukuru tumeingia kwenye hatua hii kama yalivyokuwa malengo yetu, Yanga kwa sasa ni miongoni mwa timu kubwa Afrika, tuna kikosi kipana cha wachezaji wenye uwezo unaolingana, hatuiogopi au kuihofia timu yoyote kwenye hatua inayofuata, tupo tayari,” alisema Gamondi.

Aidha, aliweka wazi kuwa analijua soka la Afrika na tayari amekushakutana na timu kubwa tangu akiwa anafundisha soka Afrika Kusini, hivyo hana cha kuhofia.

“Msimu uliopita tulipangwa kwenye kundi gumu na timu kama Al Ahly, CR Belouizdad na bado tulifanikiwa kusonga mbele kuingia hatua ya robo fainali, sina hofu ya kukutana na timu yoyote,” alisema Gamondi.

Katika hatua nyingine, Gamondi amewashukuru mashabiki wa klabu hiyo kwa namna walivyoisapoti timu yao kwenye hatua iliyopita.

“Ni jambo la kujivunia, ushindi huu umechangiwa na mashabiki wa timu hii, wamekuwa karibu na timu yao kila inapokwenda, kazi yetu ni kuhakikisha tunawapa furaha siku zote,” alisema Gamondi.

Sina tatizo na Dube

Kwa mara nyingine Gamondi amesema kukosa magoli kwa mshambuliaji wake, Prince Dube, ni jambo la kawaida kwenye mpira na anaamini atarejea kwenye ubora wake siku chache zijazo.

Dube juzi aliingia kipindi cha pili ambapo alipoteza nafasi kadhaa za kufunga kwenye mchezo huo walioibuka na ushindi wa mabao 6-0.

“Kama mnakumbuka Dube alikuwa hajacheza kwa muda mrefu wakati alipokuwa na mgogoro na klabu yake ya awali, kukosa magoli ni jambo la kawaida sana kwenye mpira, nimekuwa nikimwambia asiuzunike, taratibu atarejea kwenye makali yake, ni mshambuliaji mzuri na mwenye uwezo mkubwa,” alisema Gamondi.