Gamondi atamba kuanza ligi kibabe

By Adam Fungamwango ,, Somoe Ng'itu , Nipashe
Published at 07:14 AM Aug 29 2024
Kocha Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi.
Picha: Mtandao
Kocha Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi.

BAADA ya kutoa 'dozi nzito' katika mashindano ya kimataifa, Yanga inatarajia kuanza rasmi kutetea ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa kuwakabili wenyeji Kagera Sugar katika mechi itakayochezwa leo kwenye Uwanja wa Kaitaba ulioko Bukoba mkoani Kagera.

Yanga iliyoichapa Vital'O ya Burundi jumla ya mabao 10-0, Azam FC na Coastal Union zimechelewa kuanza Ligi Kuu Tanzania Bara kutokana na kukabiliwa na mechi za awali za mashindano ya kimataifa yanayosimamiwa na kuandaliwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF).

Akizungumza na gazeti hili jana, Kocha Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi, alisema wanawafahamu vyema wapinzani wao Kagera Sugar kuwa ni timu nzuri na ngumu.

Gamondi alisema mechi hiyo haitakuwa nyepesi kwa sababu wanaenda kukutana na moja ya timu ngumu katika Ligi Kuu Tanzania Bara na yenye wachezaji wazoefu.

Kocha huyo alisema anafahamu na anakumbuka vizuri Kagera Sugar ilivyowasumbua katika mechi ya mzunguko wa kwanza msimu uliopita ambayo ilichezwa Mei 12, mwaka jana, ambapo ilimalizika kwa sare ya bao 1-1, tena ikichezwa kwenye uwanja huohuo.

"Kagera Sugar naifahamu, ni timu ngumu, tunaiheshimu, tumejiandaa kwa ajili ya kupambana na timu ya aina hiyo, ikizingatia tunacheza ugenini na timu hii kwenye uwanja ambao ni mgumu, hatujauzoea na hata ubora wake si mzuri sana ingawa ni wa nyasi bandia, lakini sisi tuna uzoefu," alisema Gamondi.

Aliongeza anahitaji kuanza msimu mpya kwa ushindi kwa sababu anataka kufikia malengo yake kama timu na wakati wote atacheza kwa kuwaheshimu wapinzani wao.

Nahodha Msaidizi wa Yanga, Dickson Job, amekiri wanatarajia mchezo huo utakuwa mgumu kutokana na aina ya timu zinazokutana.

Job alisema kila mchezaji yuko tayari kwa mechi hiyo na wanaamini wanaenda kuendeleza furaha kwa wanachama na mashabiki wao.

"Mchezo utakuwa mgumu kwa sababu kwanza tunacheza ugenini, lakini wenzetu walifungwa mechi iliyopita kwa hiyo wanataka kushinda katika mchezo huu wa pili, sisi pia tunataka kushinda kwa sababu ni mchezo wa kwanza kwetu kwenye ligi haitapendeza kama hatutapata matokeo mazuri zaidi ya hayo," alisema Job.

Naye Kocha Mkuu wa Kagera Sugar, Paul Nkata, aliliambia gazeti hili wanakwenda kucheza na timu kubwa iliyofanya vyema katika mechi za kimataifa, hivyo wataingia  kwa tahadhari kubwa.

Nkata alisema amewaandaa wachezaji wake kucheza kwa nidhamu na kutowapa nafasi nyota wa Yanga kumiliki mchezo kwa sababu itawasababishia 'hatari; upande wao.

"Tutacheza tukiwa nyumbani, lakini na timu kubwa ambayo imefanya vyema katika michezo ya kimataifa, lakini tumejipanga, yale makosa yaliyoonekana katika mchezo wetu uliopita tukapoteza tumejaribu kuyarekebisha, nadhani tutakuwa na mchezo mzuri," alisema Nkata, kocha huyo raia huyo wa Uganda.

Kagera Sugar itashuka dimbani ikiwa na kumbukumbu ya kufungwa bao 1-0 na Singida Black Stars, mechi ikichezwa hapo hapo Bukoba wakati Yanga wao walipata ushindi mnono wa mabao 6-0 dhidi ya Vital'O katika mchezo wa mkondo wa pili wa michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya awali kuwachapa magoli 4-0.

Mechi zingine za ligi hiyo zitakazochezwa leo ni kati ya KMC dhidi ya Coastal Union wakati kwenye Uwanja wa Majaliwa ulioko Ruangwa, wenyeji Namungo itawaalika Fountain Gate.

Simba yenye pointi sita ndio inaongoza ligi hiyo baada ya mechi yake ya kwanza kuwafunga Tabora United mabao 3-0 na iliposhuka tena kwenye Uwanja wa KMC iliwachapa Fountain Gate magoli 4-0.