Coastal rasmi yahamia Arusha

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 11:45 AM Oct 11 2024
Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha.
Picha: Mtandao
Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha.

HATIMAYE Coastal Union imetangaza itatumia Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha, kama uwanja wake wa nyumbani katika michezo ya Ligi Kuu Tanzania Bara kuanzia sasa.

Hii ni baada ya tetesi za muda mrefu kuwa viongozi wa timu hiyo wanataka kuipeleka timu hiyo jijini humo, badala ya Dar es Salaam, ambapo ilikuwa ikitumia viwanja vya KMC Complex na Azam Complex, kwa michezo ya nyumbani.

Coastal Union ilikuwa ikitumia viwanja hivyo kutokana na uwanja wake halisi, Mkwakwani uliopo Tanga kuwa katika matengenezo.

Taarifa iliyotowa jana na klabu hiyo ilisema wameamua kuzipeleka mechi zao jijini humo kutokana na sababu mbalimbali ambazo baadhi yake ni kuthamini mapendekezo ya wanachama na mashabiki wao na kuirudisha timu Kanda ya Kaskazini, pamoja na ombi la mashabiki wa soka wa Arusha.

Ofisa Habari wa Coastal Union, Abbas El Sabri, amesema licha ya kuhamia Arusha, lakini watarejea uwanjani wakiwa na kocha mpya ambaye watamtangaza hivi karibuni.

"Tutatumia kipindi hiki cha kalenda ya FIFA kuendelea kukipa makali kikosi chetu kwani hatukuanza vizuri, lakini pia tutarudi upya tukiwa na nguvu, benchi letu likiwa limeimarishwa tukiwa na kocha mpya, kwa sasa tunamaliza mazungumzo ya mwisho na mwalimu tunayemhitaji na ni mmoja wa makocha bora kwenye Ukanda wa Afrika Mashariki," alisema Sabri.

Alisema kocha huyo alikuwa sehemu ya waliohudhuria mchezo kati ya timu yao dhidi ya Simba uliochezwa Ijumaa iliyopita, na kumalizika kwa sare ya mabao 2-2.

"Kwa sasa yupo Tanga tunamalizia mazungumzo kabla ya kumtangaza, tumeshampa malengo yetu na ameyakubali," alisema.

Kwa sasa nafasi ya Kocha Mkuu kwenye kikosi hicho inashikiliwa na beki wa kushoto wa zamani wa timu hiyo, Joseph Lazaro.