KLABU za Coastal Union, Mashujaa FC na Prisons, zimeanzisha timu za mpira wa miguu kwa wanawake katika kile kinachoelezwa kuwa ni matakwa ya kikanuni ya leseni za klabu siku za usoni.
Kuanzishwa kwa timu hizo kunafanya timu za Ligi Kuu Tanzania Bara ambazo pia zina vikosi vya soka la wanawake kufikia nane.
Klabu ya Coastal, imeanzisha timu yake inayoitwa Coastal Ladies ambayo kwa sasa inashiriki Ligi ya Mkoa wa Tanga ambapo wikiendi hii ilitoa kipigo cha mabao 24-0 dhidi ya Mwambao Gold, mechi ikichezwa, Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.
"Matarajio yetu ni kupanda hadi Ligi Kuu ili kwenda kutoa ushindani dhidi yaa timu kubwa za huko," alisema Abass El Sabri ambaye ni Ofisa Habari wa Klabu ya Coastal Union.
Klabu ya Mashujaa FC imetangaza kuichukua timu ya Amani Queens iliyoshuka daraja msimu uliopita na sasa itajulikana kama Mashujaa Queens.
Timu hiyo itashiriki Ligi Daraja la Pili msimu huu, ikiwa kwenye mkakati wa kurejea Ligi Kuu ya Wanawake msimu ujao.
Klabu ya Prisons inayomilikiwa na Jeshi la Magereza nayo imeanzisha timu ya soka wanawake, Prisons Queens ambayo kwa sasa ipo kambini ikijiandaa kushiriki Ligi ya Wanawake Mkoa wa Mbeya.
Taarifa iliyotolewa na klabu hiyo imeeleza timu hiyo iko chini ya Kocha Mkuu, Roland Malambi, na lengo ni kuthamini na kukuza vipaji vya soka kwa akina dada.
"Malengo yetu kwa sasa ni kupandisha timu Ligi Kuu na baadaye kuchukua ubingwa," ilisema taarifa hiyo.
Kabla ya timu hizo tatu kuwa na timu za wanawake, timu za Ligi Kuu ambazo zilikuwa na vikosi vya wanawake ni Geita Gold Queens, JKT Queens, Yanga Princess, Simba Queens, na Baobab Queens ambayo inamilikiwa kwa ubia na Azam FC.
Mkurugenzi wa Ufundi wa TFF, Salum Madadi, wakati akiwa Mkurugenzi wa Mashindano, alisema baada ya Shirikisho la Mpira wa Miguu (CAF), kuzitaka timu zote zinazocheza michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho kuwa na timu za wanawake, TFF nayo misimu michache baadaye itakuja na kanuni hiyo ya kuzitaka timu zinazocheza Ligi Kuu kuwa na timu za wanawake.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED