HUKU ikijiandaa kuwakabili mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, uongozi wa Azam FC umetangaza rasmi umempa mkataba mpya wa mwaka mmoja mshambuliaji wake, Abdul Suleiman 'Sopu'.
Taarifa iliyotolewa na Azam jana inasema sasa mshambuliaji huyo ataendelea kuitumikia klabu hiyo hadi mwaka 2026.
"Tunapenda kutangaza rasmi Sopu atakuwa katika klabu yetu hadi mwaka 2026, hii ni baada ya kumpa mkataba wa nyongeza wa mwaka mmoja," ilisema taarifa rasmi ya klabu hiyo.
Sopu alisajiliwa na Azam FC mwaka juzi akitokea Coastal Union ya jijini Tanga baada ya kuonyesha kiwango bora katika msimu wa 2021/2022.
Nyota huyo alikamilisha mazungumzo ya kujiunga na Azam siku chache baada ya kumalizika kwa Fainali ya Ngao ya Jamii iliyowakutanisha Coastal Union dhidi ya Yanga, akifunga hat-trick na kupelekea mchezo huo kwenda hatua ya matuta.
Kikosi cha Azam kilichoko chini ya Kocha Mkuu, Rachid Taoussi, kinaendelea na mazoezi ili kujiimarisha kwa ajili ya kukutana na Yanga katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara itakayochezwa kesho kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.
Yanga ndio vinara wa ligi hiyo wakiwa na pointi 24 wakifuatiwa na Singida Black Stars yenye pointi 22 huku Simba yenye pointi 21 ikifuatia katika msimamo huo wenye timu 16.
Azam iko katika nafasi ya nne ikiwa na pointi 18 huku Kagera Sugar, Pamba Jiji na KenGold zenye pointi tano kila moja zikiburuza mkia.
Ligi hiyo inaendelea leo kwa Maafande wa Mashujaa kuwakaribisha Simba kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika mkoani, Kigoma.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED