KLABU ya Azam FC, imesema inaendelea kusherehekea ushindi wao wa bao 1-0 ilioupata Jumamosi iliyopita dhidi ya Yanga na itafanya hivyo hadi Novemba 23, mwaka huu, itakapocheza mechi yake nyingine ya Ligi Kuu dhidi ya Kagera Sugar.
Ofisa Habari wa timu hiyo, Hasheem Ibwe, jana alisema kwa bahati nzuri baada ya kuwafunga Yanga hawana mchezo mwingine wowote hadi Novemba 23 itakapocheza dhidi ya Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam, hivyo wataendelea kuutumia muda huo kuendelea kusherehekea ushindi huo.
Aliwataka wanaowabeza kuendelea kushangilia ushindi huo wawaache kwani wanafanya hivyo si kwa sababu wameifunga Yanga, bali pia wamechukua pointi tatu kwa timu wanayogombea nayo ubingwa, vile vile kuwalipia kisasi wote ambao walifungwa na timu hiyo.
"Sherehe zetu bado zinaendelea tangu Jumamosi tumeendelea kufurahia ushindi dhidi ya Yanga, hakuna wa kutupangia ziendelee hadi lini, vibonzo na utani kwenye mitandao ya kijamii vitaendelea kuwapo, wasituchoke, hayo maumivu wanayopata ndiyo ambayo huwa wanayapata wenzao wanapowafunga.
"Tunafanya hivi kwa sababu si tu kwamba tumeifunga Yanga, lakini tumewafunga Mabingwa Watetezi kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara, tumeifunga timu ambayo inausaka ubingwa, ukiwa unatafuta ufalme wa soka lazima umfunge yule mnaousaka naye, unakuwa umeshampunguza nguvu na wewe umechukua pointi tatu kutoka kwake.
"Pili Yanga ndiyo mtemi wa wengine, amezifunga timu nyingi tena kubwa, halafu ni timu ambayo ilikuwa haijapoteza mchezo wowote na haijaruhusu bao, yote hayo sisi tumetibua rekodi, kwa nini tusisherehekee wiki nzima? Alitamba Ibwe.
Alisema sherehe hizo zitaendelea hadi Novemba 23, huku wakiwa wamewapa mapumziko wachezaji wao, lakini watarejea tena kwa ajili ya kuanza mazoezi kujiandaa na michezo miwili ya Novemba.
"Baada mechi dhidi ya Yanga, tuna michezo miwili mwezi huu, Novemba 23 dhidi ya Kagera Sugar na Novemba 27 dhidi ya Singida Black Stars, ni michezo migumu, lakini wachezaji wetu kwa sasa wana ari ya ushindi," alisema.
Azam iliyokuwa mgeni kwenye Uwanja wao wa Azam Complex kikanuni, ilipata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Yanga, lililowekwa wavuni na Gibiril Sillah na kuifanya kufikisha pointi 21 kwa michezo 10 iliyocheza ikiwa kwenye nafasi ya nne ya msimamo wa Ligi Kuu.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED