Azam kumrudisha Manula, yatangaza kifaa kingine

By Somoe Ng'itu ,, Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 12:50 PM Jul 01 2024
Golikipa wa Simba, Aishi Manula.
Picha: Mtandao
Golikipa wa Simba, Aishi Manula.

WAKATI ikimtangaza rasmi kiungo mshambuliaji, Nassor Saadun kutoka Geita Gold, Klabu ya Azam imetajwa kuwa katika harakati ya kumrudisha golikipa wa Simba, Aishi Manula, atakayekwenda kwa mkopo.

Habari zilizopatikana kutoka ndani ya klabu hizo mbili zinasema kumekuwa na mazungumzo ya pande mbili kuhusu kipa huyo ambaye aliwahi kuichezea Azam FC na kujiunga na Simba 2017.

Taarifa zinaeleza kuwa Azam inamhitaji Manula kutokana na uzoefu wake kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, huku viongozi wa Simba wakitaka kumuondoa ili kumsogeza Ali Salim kuwa kipa namba mbili na baadaye kumpa mikoba ya kuwa namba moja.

"Tuna kipa mzuri, Mohamed Mustapha, lakini Manula atatufaa zaidi kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa, amecheza kwa kiwango kikubwa na kuifikisha Simba robo fainali mara tano, uzoefu wake ndiyo tunaouhitaji kwa sababu sisi lengo letu namba moja angalau kwanza tutinge hatua ya makundi, tumeona atatufaa na kwetu ni rahisi kumpata, pia ni mtoto wa nyumbani," alisema mtoa taarifa kutoka Azam FC.

Taarifa kutoka ndani ya Klabu ya Simba zinasema mabosi wa timu hiyo wanaona sasa ni wakati wa kuanza maisha mapya bila ya Manula ambaye mkataba wake unamalizika 2025, hivyo kumtoa kwa mkopo.

Habari zinasema awali ilikuwa apelekwe Singida Black Stars, lakini Azam imeonyesha nia ya kutaka kumchukua, hivyo mazungumzo yanaendelea ambapo huenda Simba nayo ikanufaika na dili hilo kwa kupata mchezaji.

"Salim ni kipa mzuri na mdogo, anatunzwa ili awe kipa namba moja wa Simba, na hata Taifa Stars, moja kati ya mipango ya kumfanya afikie huko ni kumuondoa Manula ambaye kwa sasa amepoteza imani kwa wanachama na mashabiki, bahati nzuri Ayoub Lakred ambaye amezolea sifa kwa mashabiki anabaki, Salim atakuwa kipa namba mbili, Hussein Abel yeye atakuwa kipa wa tatu," kilisema chanzo.

Wakati huo huo, uongozi wa Azam FC umemsajili kiungo, Nassor Saadun kutoka Geita Gold ya mkoani Geita.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Azam, Abdulkarim Amin 'Popat', aliliambia gazeti hili jana Saadun amepewa mkataba wa mwaka mmoja na wenye kipengele cha kuongeza tena muda kama huo endapo wataridhishwa na kiwango chake.

Popat alisema wanaendelea kuboresha kila idara katika timu yao kwa sababu wanataka kufanya vema katika mashindano yote watakayoshiriki kwenye msimu mpya.

"Tunaendelea kujiimarisha kwa sababu hatutaki kurudia makosa ya miaka ya nyuma, tunataka kupata matokeo bora na kufanya vizuri katika kila michuano tutakayotia mguu wetu," alisema Popat.

Aliongeza kuwa maandalizi ya kambi yao ya Morocco yamekamilika na kinachosubiriwa ni muda wa safari kufika.

Azam pia imetangaza kumpa mkataba wa mwaka mmoja mtaalamu wa Tiba ya viungo wa wachezaji ambaye ni raia wa Brazil, Romulo De Oliveira Freitas.

Mbrazili huyo amewahi kukiongoza kikosi cha Timu ya Taifa ya Wanawake ya Ufaransa kilichoshiriki fainali za Kombe la Dunia zilizofanyika mwaka 2019 na katika klabu mbalimbali nchini China, Saudi Arabia, Kazakhstan na nchini kwao.