Viongozi wajitosa kuchangia ujenzi wa sekondari ya kisiwa cha Rukuba

By Sabato Kasika , Nipashe
Published at 12:49 PM Jul 03 2024
Baadhi ya wakazi wa kisiww cha Rukuba wakishiriki ujenzi wa secondari ya kisiwa hicho.
Picha: Kasika
Baadhi ya wakazi wa kisiww cha Rukuba wakishiriki ujenzi wa secondari ya kisiwa hicho.

VIONGOZI mbalimbali wa Wilaya ya Musoma mkoani Mara, wamejitosa kuchangia ujenzi wa shule ya sekondari ya kisiwa cha Rukuba ili ikamilike haraka na kufunguliwa Januari mwaka ujao.

Baadhi ya viongozi hao ni mkuu wa wilaya hiyo, Dk. Khalfan Haule aliyechangia Sh. 500,000, Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya hiyo, Nitu Palela aliyechangia mifuko 20 ya saruji.

Hayo yamesemwa na mbunge wa Musoma Vijjini Profesa Sospeter Muhongo ambaye amesema kuwa yeye amechangia mifuko 150 ya saruji, huku Fedha za Mfuko wa Jimbo zinunua mifuko 205 ya saruji.

"Wakazi wa kisiwa cha Rukuba wamedhamiria kufungua sekondari yao mwaka ujao, hivyo sisi viongozi tumeunga mkono juhudi hizo ili shule hiyo ifunguliwe kama walivyokusudia," Prof. Muhongo amesema.

Mbunge huyo a|mefafanua kuwa ujenzi wa sekondari hiyo ulianza miezi michache iliyopita baada ya yeye kwenda kisiwani kuhamasisha na kuanza kuchangia fedha za ujenzi kupitia harambee.

"Michango ya awali ya kuanza ujenzi imetolewa. Wakazi wa kisiwa cha Rukuba na wadau wao wa maendeleo, wamechangia fedha taslimu Sh. 1,708,000, mifuko 72 ya saruji, kokoto za Sh. 804,000, fedha za fundi Sh. 2,300,000, fundi wa kufyatua matofali Sh. 500,000," amesema.

Moja ya majengo ya madarasa.
Amefafanua kuwa nguvukazi ya wakazi wa kisiwa hicho inatumika, kwa ajili ya kusomba maji, mchanga na kuchimba msingi wa madarasa, na kwamba kazi inaendeleaa vizuri.

"Jimbo letu lina lina kata 21 zenye jumla ya vijiji 68 na sekondari 28 zikiwamo 26 za kata na mbili za binafsi. kwa sasa zinaendelea kujengwa sekondari nyingine mpya katika vijiji mbalimbali," amesema.

Mbali na Rukuba amevitaja vijiji vitatu vinavyoendelea na ujenzi wa sekondari kuwa ni Nyasaungu, Muhoji na Kurwaki, na kwamba, lengo ni kuhakikisha shule zote zinafunguliwa Januari mwaka ujao.

"Lakini pia kuna ujenzi wa sekondari mpya kwa kutumia fedha za serikali kuu ambao utaanza hivi karibuni katika Kata ya Nyamrandirira (kijijini Kasoma) na Kata ya Bukima (kijijini Butata)," amesema.

Aidha, amesema, ujenzi wa maabara tatu za masomo ya sayansi kwa kila sekondari ya kata unaendelea, na kwamba unafanikishwa kwa michango kutoka serikalini, na kutoka kwa wanavijiji na viongozi wao.

"Vilevile, kuna ujenzi wa sekondari nyingine nne mpya utakaoanza kujengwa kwa kutumia michango ya wananchi, wameniomba nikafanye harambee za kuanza ujenzi kwenye vijiji vya Mmahare, Kiriba, Kataryo na Chitare, bitafanya harambee kuanzia Julai hadi Agosti," amesema.