Itungwe sheria kali kuwadhibiti wabadhirifu wa fedha za umma

Nipashe
Published at 09:22 AM Mar 27 2024
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
PICHA: IKULU
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

TAARIFA kuhusu ubadhirifu, wizi na uchepushaji wa fedha katika mamlaka za serikali za mitaa nchini, zimekuwa zikiripotiwa mara kwa mara huku zikionyesha kwamba baadhi ya wahusika wanachukuliwa hatua kwa mujibu wa kanuni na taratibu za utumishi wa umma.

Kwa ujumla kuendelea kuwapo watu hao na vitendo kama hivyo kujirudia kila uchao, kunakwamisha nia njema ya serikali kupeleka fedha katika halmashauri kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo.  Fedha hizo ambazo zimekuwa zikiripotiwa kuibwa baadhi ni zile za mapato ya ndani katika halmashauri na zingine kutoka serikali kuu zinazotolewa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi kama afya, elimu, barabara na maji. 

Kila viongozi wa juu kama Rais, makamu wa Rais na Waziri Mkuu wanapofanya ziara katika maeneo mbalimbali kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo, mambo hayo yamekuwa yakiripotiwa na wahusika kuchukuliwa hatua. Pamoja na hatua zinazochukuliwa, inaonekana kuwa tatizo hilo ni sawa na ugonjwa sugu kwa kuwa watu wamekuwa wakiendelea kutumbua tu fedha za umma. 

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, alipofanya ziara mkoani Kigoma, aligundua wizi wa kutisha wa fedha za miradi huku baadhi ya miradi iliyopewa fedha hizi imetekelezwa chini ya kiwango. Bila kusita, Waziri Mkuu aliagiza wahusika wote wachukuliwe hatua ikiwamo kuchunguzwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria. 

Kama vile haitoshi, alipofanya ziara mkoani Mara, mambo kama hayo yalijirudia na mbaya zaidi ikabainika kuwa baadhi ya watendaji hao ngazi ya halmashauri, wana mtandao wa ushirikiano na maofisa katika Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI). Hiyo ilibainika baada ya ofisa mmoja aliyechukua fedha na kukutana na maofisa wa TAMISEMI katika mji mmoja kisha kugawana.

Jambo hilo la kuwapo kwa mtandao baina ya baadhi ya watendaji wa halmashauri na maofisa wa TAMISEMI limebainika baada ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) kutoa kauli hiyo ikiwa katika ziara Muheza mkoani Tanga. Kamati hiyo imebainisha wazi kwamba baadhi ya maofisa katika ofisi hiyo ya Rais wanawalinda wabadhirifu wa fedha kwenye halmashauri kwa kuwakumbatia ili wasichukuliwe hatua. 

Mwenyekiti wa LAAC, Halima Mdee, alisema hayo mwishoni mwa wiki iliyopita wakati akifanya majumuisho ya ziara kwa kuzungumza na watumishi wa halmashauri baada ya kukagua ujenzi wa shule ya sekondari na hospitali ya wilaya. Alisema hali hiyo ya kulindana inatokana na uswahiba baina ya watumishi wa TAMISEMI na halmashauri na huo ni mtandao wa kuiba fedha za umma zinazotolewa kwa ajili ya miradi ya maendeleo. 

Kwa ujumla, hadithi ya kuwapo kwa ubadhirifu wa fedha katika halmashauri si mpya kwa kuwa imekuwa ikielezwa kila mwaka na hata ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka husika, zimekuwa zikijirudia. 

Hatua hiyo inaonyesha kwamba tatizo hilo ni sugu na halijapatiwa ufumbuzi wa kudumu. Hali hiyo imekuwa ikisababisha miradi mingi ya serikali kufanyika katika kiwango duni na mingine kutokukamilika na matokeo yake wananchi kuendelea kupata adha ya ukosefu wa huduma mbalimbali. 

Wahenga wanasema penye nia pana njia. Kwa mantiki hiyo kama kweli kuna nia ya dhati ya kukomesha vitendo kama hivyo, hapana budi kuchukuliwa hatua dhidi ya wahusika kwa kuwa vitendo kama hivyo ni uhujumu wa Uchumi. Kwa mantiki hiyo, serikali ifanye mabadiliko ya sheria kwa kuwaingiza watu hao kwenye kundi la uhujumu uchumi. 

Ni imani kwamba kama hiyo itafanyika na wahusika wa wizi na ubadhirifu wa mabilioni ya shilingi za serikali wakafikishwa mahakamani na kuhukumiwa, ni wazi kwamba kutakuwa na mabadiliko makubwa. Watu wanaopewa dhamana ya kusimamia fedha hizo watakuwa na nidhamu wakiamini kwamba wakifanya makosa, sheria itawahusu.