Hatua stahiki zichukuliwe katika kukabiliana na vitendo hivi viovu

Nipashe
Published at 03:15 PM Mar 28 2024
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamadi Masauni.
PICHA: CCM
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamadi Masauni.

TANZANIA imekuwa ikichukua tahadhari mbalimbali dhidi ya matishio yanayoweza kujitokeza yakiwamo ya ugaidi hasa kutokana na kuwapo kwa vikundi vinavyojihusisha na vitendo hivyo katika nchi jirani. Miongoni mwa hatua hizo ni kutungwa kwa Sheria ya Kupambana na Ugaidi ya Mwaka 2022 ambayo msukumo mkubwa ulitokana hasa na uvamizi wa ofisi za ubalozi Dar es Salaam na Nairobi, Kenya mwaka 1998.

Aidha, katika kupambana na vitendo hivyo kwa kuzingatia kuwa inapakana na mataifa mbalimbali, Tanzania kupitia vyombo vyake vya ulinzi na usalama, imekuwa ikiweka ulinzi wa kutoka kwenye maeneo ya mipaka. Lengo ni kuhakikisha viashiria vya vitendo vyovyote vya kigaidi pamoja na uingiaji wa wahamiaji haramu vinadhibitiwa na kukomeshwa. 

Pamoja na kujizatiti huko, taarifa iliyotolewa karibuni inaonyesha kuwa Tanzania haina mifumo  mizuri ya usimamizi na ufuatiliaji wa mienendo wa jumuiya za kiraia zikiwamo taasisi na madhehebu ya dini. Hali hiyo inasababisha kuwapo kwa hatari ya taasisi hizo hasa madhehebu ya dini  kutumika katika utakatishaji fedha haramu au kufadhili masuala ya kigaidi.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamadi Masauni, alibainisha hayo wakati wa uzinduzi wa kampeni za usajili wa jumuiya huku akiweka bayana kwamba baadhi ya jumuiya za kiraia zimeripotiwa kujihusisha au kutumika katika kufanikisha kutendeka kwa makosa ya jinai na vitendo vingine vyenye madhara kwa jamii.

Miongoni mwa makosa hayo, kwa mujibu wa Waziri Masauni ni utakatishaji wa fedha haramu, ugaidi na ufadhili wa shughuli za kigaidi, usafirishaji haramu wa binadamu, biashara haramu ya silaha na uwapo wa jumuiya za kidini zinazotoa mafundisho potofu na hatarishi kwa usalama wa raia (afya ya mwili na akili). 

Kutokana na kuwapo kwa taasisi hizo, alisema hali hiyo imesababisha Tanzania kuwekwa katika kundi la nchi zinazohitaji ufuatiliaji wa karibu. Pia hali hiyo inaharibu taswira nzuri ya Tanzania katika  medani ya diplomasia ya kimataifa iliyopo sasa. 

Kuna msemo kwamba ukiona panafuka moshi ujue pana moto au unapodhania pana amani, uharibifu upo. Taarifa hiyo inabainisha kwamba Tanzania si nchi salama kwa kiwango cha juu kama inavyoaminika bali kuna viashiria vya kuwapo matendo maovu yakiwamo ya kigaidi. Kwa mantiki hiyo, taarifa hiyo inatuamsha kutoka usingizini kwamba tunapaswa kuamka na kuchukua tahadhari. 

Ni kweli kwamba hivi sasa kumeibuka madhehebu mengi ya dini hata katika maeneo ya makazi na wengine wanafanya ibada katika vituo vya mabasi. Jambo la kujiuliza je, mafundisho yanayotolewa na wahubiri hao yanafuata misingi ya mafundisho halisi ya dunia husika? 

Jambo lingine la kujiuliza ni kama kuna ufuatiliaji wa  kutosha kujua matendo na mienendo ya taasisi hizo. Tunasema hivyo kwa kuwa kuna uwezekano wa kuwapo viashiria vya utakatishaji fedha na mipango ya chini kwa chini kutokana na kufadhiliwa na watu ambao huenda hawana nia njema na usalama wa nchi.

Kama alivyosema Waziri, ni dhahiri kwamba kuna udhaifu katika ufuatiliaji ndiyo maana ripoti inaonyesha kwamba kuna tatizo kubwa katika  eneo hilo. Kwa mantiki hiyo, ni vyema kikaundwa kitengo cha tathmini na ufuatiliaji ili kubaini mienendo ya uendeshaji wa taasisi hizo. 

Wakati wa serikali ya awamu ya nne chini ya Rais (mstaafu) Jakaya Kikwete, baadhi ya viongozi wa dini walituhumiwa kujihusisha na biashara haramu ya dawa za kulevya. Jambo hilo pia lichukuliwe kwa uzito kama rejea na kuanza kufanyia kazi viashiria vya vitendo viovu vilivyoainishwa kwenye ripoti.  

Hali hiyo inatokana na ukweli pia kwamba baadhi ya viongozi wa madhehebu hayo badala ya kuwahubiria watu masuala ya imani, ikiwamo kutenda matendo mema na kuishi maisha yasiyo na uchochezi, wamekuwa wanafundisha masuala ya utajirisho. Ni vyema hatua zikaanza kuchukuliwa sasa kabla mambo hayajafikia hatua mbaya.