Zijue takwimu za wapinzani Simba, Yanga, Azam CAF

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 07:59 AM Jul 15 2024
Vital'O
Picha: Mtandao
Vital'O

WIKI hii, Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), liliendesha droo na kutoa ratiba ya michuano linayoisimamia, Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho.

Katika droo hiyo iliyochezeshwa Cairo nchini Misri, Yanga imepangwa kucheza dhidi ya Vital'O ya Burundi, huku Azam FC ikiangukia kwa APR ya Rwanda katika michezo ya Ligi ya Mabingwa Afrika, huku Mabingwa wa Zanzibar, JKU wakipangwa dhidi ya Pyramids ya Misri.

Coastal Union ambayo ipo Kombe la Shirikisho Afrika itacheza dhidi ya Bravos do Maquis ya Angola, huku Simba itakayoanzia moja kwa moja raundi ya kwanza mwezi Septemba dhidi ya mshindi wa mechi ya awali kati ya mwakilishi kutoka nchini Libya na Uhamiaji kutoka Zanzibar.

Katika makala haya tunakuletea historia, takwimu na rekodi za timu ambazo ni wapinzani wa Simba, Yanga, Azam, JKU na Coastal Union.   

1. Vital'O

Itakuwa nyumbani kati ya Agosti 16 na 18 kupambana na Mabingwa wa Tanzania Bara, Yanga kwenye mechi ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Wenyewe ni Mabingwa wa Burundi, wakiwa wamemaliza ligi wakivuna pointi 72 katika mechi 30 walizocheza, ambapo ligi yao ina timu 16 kama ilivyo nchini.

Ilimaliza ikiwa imeshinda mechi 22, sare sita, ikipoteza mara mbili, ikipachika mabao 52 na kuruhusu 11.

Itacheza na Yanga, ambayo nayo kwenye ligi yake yenye timu 16, imevuna pointi 80, ikicheza mechi 30, kushinda 26, sare mbili na kupoteza mbili, ikipachika mabao 71 na kuruhusu wavu wake kuguswa mara 14.

Vital'O, iliyoanzishwa mwaka 1957, iliamua kujiita jina hilo 1975, baada ya kupitia majina kadhaa kama Gwanda, Sport FC miaka ya 1960, na kuanzia 1971, ikaitwa Atletico, baadaye ikabadilishwa na kuitwa Tout Puissant Bata mwaka 1973, jina ambalo halikukaa sana, ikajipachika tena jina la Espoir FC, ambalo nalo waliona halifai na hatimaye 1975, wakajiita Vital'O ambalo limeishi hadi leo.

Timu hiyo imetwa ubingwa wa nchi mara 20, Kombe la Burundi ambalo ni kama FA Cup kwa hapa nchini, mara 14.

Imetwaa Ubingwa wa Afrika Mashariki na Kati, maarufu kama, Kombe la Kagame mara tatu, huku mafanikio yao makubwa kwenye michuano ya kimataifa ni kufika hatua ya fainali ya Kombe la Washindi barani Afrika (sasa Kombe la Shirikisho Afrika), 1992 na kufungwa jumla ya mabao 5-1 dhidi ya African Sports ya Ivory Coast, ikitoka sare ya bao 1-1 nyumbani na kukong'otwa mabao 4-0 ugenini. 

2. APR FC

Kwa sasa ipo nchini Tanzania, ikishiriki michuano ya Kombe la Dar Port Kagame, inayoendelea kwenye viwanja vya KMC, Mwenge, Dar es Salaam na Azam Complex, Chamazi.

Timu hii inayomilikiwa na Jeshi la Rwanda, jina lake kamili ni Armee Patriotique Rwandaise, na kila herufi ya mwanzo ya maneno hayo, ndiyo unapata jina la APR.

Itakumbana na Azam FC, katika mchezo wa awali wa Ligi ya Mabingwa Afrika, Azam ikianzia nyumbani kati ya Agosti 16 na 18,  marudiano yatafanyika Kigali, nchini Rwanda kati ya tarehe 23, mpaka 25 mwezi huo, kusaka timu itakayokwenda raundi ya kwanza ya michuano hiyo.

Ndiyo mabingwa wa nchi hiyo kwa sasa, wakiutwaa kwa kukusanya pointi 68, ambapo kwa michezo 30 iliyocheza, ilishinda 19, sare 11 na haikupoteza mechi yoyote ile katika ligi hiyo iliyokuwa na timu 16.

Itacheza na Azam ambayo yenyewe ilimaliza Ligi Kuu Bara ikiwa katika nafasi ya pili na pointi 69.

Imetwaa ubingwa wa Ligi Kuu mara 22, na Kombe la Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini Rwanda, mara 13.

Kama itatwaa Kombe la Kagame mwaka huu basi itakuwa mara ya nne, kwani imeshawahi kufanya hivyo, mwaka 2004, 2007 na 2010.

Haijawahi kuingia kwenye makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika tangu ianzishwe mwaka 1993, lakini mafanikio yao makubwa kwenye michuano ya kimataifa ni kufika hatua ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika mwaka 2003, ilipotolewa na Julius Berger ya Nigeria, kwa jumla ya mabao 3-2, ambapo ilibamizwa mabao 3-0 ugenini, na kushindwa kusonga mbele licha ya kushinda mabao 2-0 nyumbani mechi ya marudiano.

 3. Pyramids FC

Ni moja kati ya timu bora kwa sasa barani Afrika ambayo kwa sasa inaongoza Ligi Kuu nchini Misri ikiwa na pointi 68, ikiwa imecheza mechi 28, ikishinda 21, sare tano na kupoteza mbili, ikifuatiwa na Al Ahly ambayo ina pointi 60, lakini ikiwa imecheza michezo 24.

Itacheza na Mabingwa wa Zanzibar, JKU, ambayo imemaliza ligi msimu uliopita ikikusanya pointi 66 kwa michezo 30 iliyocheza.

Ikumbukwe kuwa mshindi wa mechi hii ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika ndiye atakayecheza dhidi ya mshindi kati ya Azam FC dhidi ya APR ya Rwanda.

Pyramids ilianzishwa 2008 ikijulikana kama Al Assiouty Sport, kabla ya kubadilisha jina baadaye. Haijawahi kutwaa ubingwa wa Misri, lakini ilimaliza nafasi ya pili misimu ya 2018/19 na 2021/22, mshindi wa pili ya makombe ya FA, 2018/19 na 2021/22 na Super Cup ya nchini hiyo 2022/23.

Mafanikio yake makubwa zaidi mechi za kimataifa ni kufika hatua ya fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu wa 2019/20 ilipofungwa bao 1-0 dhidi ya RS Berkane ya Morocco katika mechi ya mkondo mmoja tu, iliyochezwa nchini Morocco.

 4. Bravos do Maquis

Ni timu ngeni kwa masikio ya mashabiki wa soka nchini Tanzania. Inatoka nchini Angola ambapo itacheza dhidi ya Coastal Union kwenye Kombe la Shirikisho Afrika, kuania Agosti 16 hadi 18, nyumbani, kabla ya kuwafuata wapinzani wao nchini Tanzania katika mechi ya marudiano.

Imemaliza nafasi ya nane kwenye msimamo wa Ligi Kuu nchini Angola ikiwa na timu 14, ikicheza mechi 28,  ikivuna pointi 37.

Bravos do Maquis ilianzishwa 1983, haina mafanikio yoyote kimataifa, wala nchini kwao, ambapo mwaka 2015 ilitwaa Kombe la FA, na mwaka unaofuata ikafika fainali ya Super Cup. Itachezwa na Coastal Union iliyomaliza Ligi Kuu ikiwa nafasi ya nne ikiwa na pointi 43.

 5. Uhamiaji/ Libya

Simba ndiyo timu pekee itakayocheza mechi yake ya kwanza Septemba mwaka huu kwani haitocheza kwenye raundi ya awali, kutokana na kuwa ndani ya timu 10 bora za Afrika.

Katika droo iliyopangwa, itacheza moja kwa moja raundi ya kwanza ya Kombe la Shirikisho Afrika na mshindi kati ya Uhamiaji ya Zanzibar na timu moja kutoka nchini Libya, ambako ligi hiyo inaendelea.

Kutokana na msimamo wa ligi nchini humo ilivyo, timu tano ambazo zinatarajiwa kucheza dhidi Uhamiaji ya Zanzibar na mshindi wake atapambana na Simba ni Al Ahly Tripoli, Al Nasr, Al Hilal Benghazi, Al Ahly Benghazi, na Al Madina.

Uhamiaji ni timu iliyoshika nafasi ya sita kwenye msimamo wa Ligi Kuu Zanzibar iliyomalizika, ikikusanya pointi 47 katika michezo 30 iliyocheza.

Uhamiaji imepata nafasi ya kuiwakilisha Zanzibar katika michuano hiyo baada ya Chipukizi FC, timu iliyokuwa imefuzu kucheza kujiondoa kutokana na ukata.