Vyuo vya afya nchini kuanza kutumia mtalaa mmoja wa mafunzo- Msofe

By Imani Nathaniel , Nipashe
Published at 06:23 AM Aug 27 2024
Mkurugenzi wa Elimu ya Juu kutoka Wizara ya Elimu, Sanyansi na Teknolojia Profesa Peter Msofe

Mkurugenzi wa Elimu ya Juu kutoka Wizara ya Elimu, Sanyansi na Teknolojia Profesa Peter Msofe amesema hivi karibuni utaanza kutumika mtalaa mmoja kwa wanafunzi wa masomo ya udaktari na uuguzi, lengo likiwa kupata wahitimu wenye sifa moja na washindani katika soko la ajira ndani na nje ya nchi.

Pia kuanza kutumika kwa mtalaa huo kutawaongezea wakufunzi wa fani hizo ujuzi pamoja na kuwezesha mgonjwa kupata huduma bora na inayofanana kwa kila mtaalamu.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Kongamano mapema jana, Msofe, alisema kuwa , kuanza kutumika kwa mtaala huo unalenga kuwaongezea wakufunzi  ujuzi pamoja na kumuwezesha mgonjwa kupata huduma bora na inayofanana kwa kila mtaalamu.

Mtalaa huo tayari umeanza kutekelezwa na Chuo kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (Muhas), Chuo Kikuu cha Afya Bugando na Chuo Kikuu cha Afya Bugando (Cuhas) pamoja na Chuo cha Afya Kilimanjaro (KCMUCo) chini ya mradi wa mabadiliko ya ufundishaji wa wataalamu wa afya ukifadhiliwa na Taasisi ya Bill and Melinda Gates.

"Mradi huu umetumika kutengeneza mitaala ya mfano katika mafunzo ya udaktari na uuguzi,mitaala hii imeshapitishwa na taasisi ya urekebu pamoja na Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) na tunatarajia mtaala huu utumike kwa vyuo vyote vya afya nchini,"alisema.

Msofe alisema mtaala huo unalenga kutengeneza namna tofauti ya ufundishaji katika masomo ya tiba katika fani ya afya.

Alisema ujio wa mtaala huo ni kutokana na mahitaji kuongezeka hivyo ufundishaji lazima ubadilike kwani miaka ya nyuma mgonjwa anapokwenda kwa daktari husubiri maelezo yote kwa daktari lakini sasa anakwenda hospitali akifahamu ugonjwa unaomsumbua.

Mkurugenzi huyo alisema ni lazima madaktari wafundishwe namna ya kuhudumia watu wa namna hiyo pamoja na kuzalishwa wahitimu wenye maarifa na uwezo wa kutumia ujuzi wao katika mazingira halisi ya kazi.

 Kwa upande wake Makamu Mkuu wa Chuo Cha Muhas Profesa Apolinary Kamuhabwa alisema mtaala huo walioutengeneza kwa ushirikiano na Chuo Kikuu Cha Duke na Chuo Kikuu Cha California San Francisco Francisco za nchini Marekani utakwenda kubadilisha ubora wa mafunzo ya afya nchini.

Profesa Kamuhabwa alisema mradi huo umepitia mitaala ya afya nchini na kuangalia namna wataalamu wa sekta hiyo wanavyofundishwa na kuainisha mambo wanayopaswa kujifunza kwa mazingira ya Tanzania na duniani.

"Mbali na mitaala tumewatengeneza wataalamu wa kuwafundisha walimu, mwalimu akiajiriwa tayari tuna wataalamu wetu wa kuwafundisha mitaala hii,"alisema.

Profesa huyo alisema utekelezaji wa mtaala huo utaanzia vyuo vya kati hadi vyuo vikuu ili kupata wataalamu wenye ujuzi usiotofautiana sokoni akisisitiza hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa malengo ya Serikali kuboresha elimu kuanzia ngazi za chini hadi vyuo vikuu.