Akina mama wajasiriamali, wenye ulemavu wapewa mafunzo

By Elizabeth Zaya , Nipashe
Published at 06:26 PM Aug 23 2024
Wakina mama wakionesha kwa vitendo namna ya kutengeneza mkaa mbadala kwa kutwanga malighafi kwenye kinu, hii ni baada ya kupata mafunzo hayo kutoka Sauti ya Jamii Kipunguni, Ukonga Dar es Salaam.
Picha: Elizabeth Zaya
Wakina mama wakionesha kwa vitendo namna ya kutengeneza mkaa mbadala kwa kutwanga malighafi kwenye kinu, hii ni baada ya kupata mafunzo hayo kutoka Sauti ya Jamii Kipunguni, Ukonga Dar es Salaam.

SAUTI ya Jamiii Kipunguni, imeendesha mafunzo kwa akina mama wajasiriamali, wa majumbani na wenye ulemavu kutoka maeneo ya Majohe na Kivule, Ilala Dar es Salaam, namna ya kutengeneza mkaa mbadala kwa ajili ya matumizi ya nyumbani na kwenye biashara zao ndogondogo hususani za kupika.

Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Mkurugenzi wa Sauti ya Jamii Kipunguni, Selemani Bishagazi, amesema mafunzo hayo ni endelevu lakini kwa awali wanataka angalau kufikia kaya 200 kutoka maeneo hayo ambazo zitafundishwa kutengeneza na kuanza kutumia mkaa huo mbadala.

Bishagazi amesema mkaa mbadala hauna gharama na unasaidia kwa kiwango kikubwa kuokoa mazingira na afya za watu.

"Mkaa huu unatengenezwa kutokana na taka ambazo wengi wetu tumekuwa tukizilipia fedha ili zipelekwe kwenye maeneo ya kutupia taka, kwa hiyo kwa sasa tunawafundisha namna ya kuzitumia taka hizo kuwa mkaa mbadala kwa ajili ya kupikia,"amesema Bishagazi.

"Hii ni teknolojia rahisi sana ambayo kila mtu nyumbani kwake anaweza kutengeneza akatumia na kuachana na matumizi ya mkaa wa kukata miti kwa kuwa mbali na kuwa unaharibu misitu na mazingira yetu lakini pia ni hatari kwa afya.

Mkurugenzi wa Sauti ya Jamii Kipunguni, Ukonga Dar es Salaam, Selemani Bishagazi(aliyesimama) akizungumza wakati wa mafunzo ya namna ya kutengeneza mkaa mbadala kwa akina mama na wenye ulemavu kutoka maeneo ya Majohe na Kivule.
"Mkaa huu mbadala kwanza hauna hatari kwa afya, hauharibu mazingira, unapika kwa muda mrefu jikoni na unasaidia kupunguza gharama za maisha,"amesema Bishagazi.

Mmoja wa waliopewa mafunzo hayo kutokea Majohe, Seya Khasad, amesema mkaa huo mbadala umekuwa mkombozi kwao kwa kuwa hauna gharama.

"Yaani sasa hivi zile taka tulikuwa tunapeleka kwenye magari ya taka kwenda kutupa ndio tunazitengeneza tunatumia kupikia, kwa hiyo tumeokoa mambo mengi sana maana hatununui tena mkaa ule wa kukata miti, hatulipi hela ya taka, tunalinda afya zetu na tunaokoa misitu yetu,"amesema Khasad.