Wakulima wa miwa wa Bonde la Kilombero wanatarajiwa kunufaika na ubunifu sambamba na teknolojia za kisasa za kilimo zitakazooneshwa kupitia maonesho ya siku ya wakulima wa miwa Kilombero, yatakayofanyika kuanzia tarehe 10 hadi 12 Oktoba 2024.
Maonesho hayo ya siku tatu yanaungwa mkono na Kampuni ya Sukari Kilombero, kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wakiwemo; Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Benki ya CRDB, Agriculture Co. Ltd, Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), Shirika la African Wildlife Foundation, Umoja wa Mataifa wa Uhifadhi wa Mazingira (IUCN), Unitrans, Kanu Equipment, na Kilombero Co-operatives Joint Enterprise Ltd.
Maonesho hayo yanalenga kuwawezesha wakulima kwa kutumia teknolojia za kisasa zinazolenga kuongeza uzalishaji, ufanisi, na kujitegemea katika sekta ya sukari.
Kwa mara ya kwanza, maonesho hayo ya mwaka huu yameongezwa kuwa ya siku tatu, na yanatarajiwa kuvutia maelfu ya wakulima wa miwa na wadau wa sekta ya kilimo.
Teknolojia mbalimbali, zikiwemo vifaa vya kilimo, mifumo endelevu ya umwagiliaji na mashine za kisasa zitaoneshwa ili kusaidia wakulima kuongeza mavuno na kupunguza athari za kimazingira na gharama za uendeshaji.
Victor Byemelwa, Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi na Meneja Mawasiliano na Mahusiano na Wadau wa Kampuni ya Sukari Kilombero, ameelezea umuhimu wa tukio hilo.. "Tumeongeza muda wa maonesho ya wakulima wa miwa Kilombero mwaka huu ili wakulima wapate fursa ya kuona ubunifu na teknolojia za hali ya juu zinavyobadili sekta ya miwa.
Teknolojia hizi zitawezesha wakulima kuongeza uzalishaji, kuboresha ufanisi, na kuifanya Tanzania kujitegemea katika uzalishaji wa sukari." amesema na kuongeza kuwa;
"Maonesho haya yatatoa vipindi vya moja kwa moja kuhusiana na masuala ya ushirikiano na semina za kiufundi zitakazoongozwa na wataalamu wa sekta ya kilimo, zikiangazia changamoto mbalimbali kama vile: - mavuno duni, gharama za juu za uzalishaji, na ushindani kwenye soko.
James Mayunga, Meneja wa Kilombero Joint Enterprises Cooperatives Society, inayowakilisha Vyama vya Ushirika vya Masoko ya Kilimo (AMCOS) 17, amesisitiza jinsi tukio hilo litavyowanufaisha wakulima wa eneo hilo.
“Maonesho haya ni fursa muhimu kwa wakulima wetu kukumbatia mbinu za kisasa za kilimo. Kwa msaada wa Kampuni ya Sukari Kilombero na washirika wengine, tunawawezesha wakulima kwa maarifa na teknolojia ili kuboresha mavuno yao, kufanya kazi kwa ufanisi zaidi, na kufikia kujitegemea,” amesema Mayunga.
Maonesho hayo yako wazi kwa wakulima wote wa miwa na wadau husika, na kushiriki ni bure. Washiriki watanufaika na shughuli mbalimbali ikiwemo maonesho ya kiufundi, ushauri wa kifedha, na fursa za kushirikiana na wadau muhimu katika sekta ya miwa.
Kwa pamoja, mashirika haya yamejipanga kuendeleza sekta ya miwa ya Tanzania kupitia ubunifu, mbinu za kilimo endelevu, na msaada wa kifedha.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED